21 Apr 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waziri atangaza harambee ya ujenzi wa hosteli za wasichana Mtwara
 
2007-04-21 18:59:51
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Hawa Ghasia, amesema wanaume wasijione ni wajanja sana kwa kuwapa wanafunzi mimba kwani hata wao wanaweza kuathirika kwa kupata ukimwi ambao huwagharimu maisha yao.

Waziri Ghasia ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akitangaza harambee ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana wilayani Mtwara itakayofanyika leo hii katika hoteli moja Jijini.

Amesema kitendo cha wanafunzi wa kike kupata mimba ni ushahidi kuwa huwa wanafanya ngono bila kujikinga na hivyo, wasichana hao na wanaume wanaowapa mimba, wote wako katika hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi.

``Wanaume wasijione ni wajanja sana. Mimba kweli watawapa wasichana, lakini ukimwi je? Lazima na wao watanasika.

Hivyo ni bora kuacha kabisa kuwafuatafuata waanafunzi na kuwakatishia masomo yao kwa kuwapa mimba,`` akasema Waziri Ghasia.

Akasema Waziri Ghasia kuwa ujenzi wa hosteli za watoto wa kike ni njia mojawapo muhimu ya kuwaepushia watoto wa kike mimba na hatimaye kuwawezesha kuendelea na masomo yao kama wanavyotarajiwa na jamii.

Aidha, Waziri huyo amekanusha kuwa ngoma za unyago zinazochezwa na wakazi wa mikoa ya kusini hususan wa mkoa wa Mtwara ndizo zinazochangia wanafunzi kupata mimba.

Badala yake, akasema ngoma hizo zina mafundisho mazuri na laiti kama watoto wote wangechezwa unyago, kamwe wasingepata mimba kutokana na vitisho wanavyopewa na wakufunzi wao wakati wa unyago.

``Mimi mwenyewe nimechezwa unyago. Lakini nimesoma na sikupata mimba wakati nikiwa mwanafuzi.

Lakini pia wapo wengine kama mama Anna Abdallah ambaye pia amechezwa unyago na akasoma… sio kweli kuwa unyago unachangia watoto kupata mamba. Cha msingi ni kuzingatia maelekezo mema na kujiepusha na ngono zembe,`` akasema Bi. Ghasia.

Akitilia mkazo katika kukanusha mtazamo potofu juu ya unyago, Waziri Ghasia amesema enzi zao, karibu Wanawake wote walikuwa wakichezwa unyago hapakuwepo na matukio mengi ya wanafunzi kupata mimba kama ilivyo hivi sasa ambapo unyago umepuuzwa.

``Mimi mpaka wakati nafika darasa la saba ndipo aliporipotiwa mwanafunzi wa kwanza kupata mimba shuleni kwetu… ilikuwa ni aibu na siri kubwa, wakati huo tulikuwa tukichezwa unyago.

``Lakini leo hii unyago hauchezwi na mimba zimekuwa nyingi. Mimi nadhani unyago sio chanzo cha watoto wa kike kubeba mamba ila kuna sababu nyingine ambazo lazima tuzijue na kupambana nazo,`` akasema.

Pia akasema ni vizuri sasa kwa ngoma hizo kuboreshwa ili zitoe elimu sahihi ya ukimwi kwa watoto wa kike na hatimaye kuwakinga na janga la ukimwi.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.