|
Niokoe jamani!
2007-04-23 19:05:38
Na Mwandishi Wetu
Tangu gazeti hili lichapishe taarifa kuhusu matatizo ya kiafya yanayomkabili mtoto Sada Mwesi Timo, wasamaria wema kutoka ndani na nje ya nchi wamejitokeza kumsaidia.
Hata hivyo bado msaada wa hali na mali unahitajika ili kuokoa maisha ya mtoto huyo ambaye ameishi kwa mateso makubwa tangu alipozaliwa miezi minane iliyopita.
Mama wa mtoto huyo, Bi. Mwanaidi Mwesi, 17, baada ya kutoa kilio chake kupitia gazeti hili Ijumaa iliyopita, na kupata visenti kidogo, alirudi kwao Moshi baada ya maisha ya Jijini Dar ya kubahatisha kuwa magumu.
Hata hivyo gazeti hili liliwasiliana naye na leo asubuhi alianza safari kurudi Jijini ili kupokea misaada ambayo imeshapatikana na pia kujadiliana na madaktari kuhusu matibabu ya mtoto wake.
Baadhi ya wasamaria waliochangia waliomba majina yao yasitajwe gazetini kwa kile walichodai kuwa wanatoa msaada huo kutokana na kuguswa na tatizo la mtoto na si kujitangaza.
Miongoni mwa waliotoa michango yao ni mtu mmoja kutoka Muscat huko Oman aliyejitambulisha kwa jina la Ahmed Zahrani ambaye kiasi alichotoa kitatangazwa baadaye kama ataridhia.
Wasamaria wema wanaopenda kutoa msaada wanaombwa kuwasilisha michango yao kwenye ofisi za gazeti hili zilizoko Mikocheni Jijini Dar es Salaam, mkabala na kituo cha televisheni cha ITV kuanzia asubuhi hadi saa 10:30 jioni. Pia wanaweza kuwasiliana na Mhariri wa gazeti hili kwa simu namba 0784 358262.
Mtoto Sada anasumbuliwa na tatizo la kupumua baada ya kuzaliwa bila kuwa na pua, hali hiyo imemfanya aishi kwa shida kubwa huku mama yake akiwa hana msaada wowote.
Baba yake Sada alitimka baada ya mkewe kujifungua mtoto mwenye matatizo ya kiafya.
|