|
Ticha afanya unyama
2007-04-23 19:09:10
Na Emmanuel Lengwa, Kawe
Wakati Serikali ikijitahidi kwa kila hali kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule nchini wanapata elimu bora, mambo yanaelekea kuwa kinyume chake katika baadhi ya shule ambapo majuzi mwalimu mmoja wa darasa la pili anadaiwa kufanya unyama usio wa kawaida, tena mbele ya darasa lake!
Mwalimu huyo wa kike , ni wa Shule ya Msingi Kawe, Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Mwalimu huyo inadaiwa Jumatano ya wiki iliyoisha alimlazimisha mtoto mmoja kunywa mkojo uliokuwa kwenye chupa ndogo ya maji huku akimlamba bakora kadhaa mwilini.
Inadaiwa kuwa wakati akifanya unyama huo mbele ya darasa, wanafunzi wengine walitulia kimya, wakihofia na wao kuangushiwa mvua ya bakora na mwalimu wao huyo anayeonekana kuwa bado hajaujua vyema uchungu wa mwana.
Alasiri baada ya kupata habari hiyo ya kustusha toka kwa baadhi ya watoto walioshuhudia mwenzao akinywa kojo, ilitua hadi kwa mwalimu huyo wa kike na kumuuliza kulikoni.
``Nimekatazwa kuzungumza… lakini ni shetani tu alinipitia,`` akasema mwalimu huyo huku akionekana mwenye hofu tele.
Tukio lenyewe linasimuliwa hivi:
Kwamba, siku hiyo Jumatano, mwalimu huyo aliingia darasani na kuanza kufundisha somo lake kama kawaida.
Mara, mtoto mmoja wa kiume akamfuata mwalimu huyo na kumuomba ruhusa ya kwenda msalani, akidai kuwa amebanwa na haja ndogo.
Mwalimu, bila kujali kuwa siku hiyo kulikuwa na kiwingu kilichowafanya watoto waende msalani mara kwa mara kwa ajili ya haja ndogo, akamkatalia mtoto huyo wa kiume.
Kwa kuwa alibanwa sana, mtoto huyo akazidi kumbembeleza mwalimu huku akijishika na kukaribia kulia, akihofia asiumbuke mbele ya wenzie.
Hapo, mwalimu akatishia kumcharaza bakora na saa hiyo hiyo akamuamuru akakae kwenye dawati lake.
Mwanafunzi akakosa la kufanya. Akaenda kuketi. Dakika chache baadaye, mtoto huyo akazidiwa na haja ndogo. Kuona hivyo, akamuomba mwenzie mmoja chupa ndogo ya maji na kumwaga kojo lote lililombana.
Darasani hakuna dogo! Mwanafunzi mmoja akapiga kelele na kumwambia mwalimu kuwa mwenzao amekojoa darasani.
Balaa likaanzia hapo. Mwalimu akamtoa mbele ya darasa mwanafunzi yule wa kiume na kumtaka anywe mkojo wake wote.
Aliposita, akaanza kumtembezea bakora mfululizo mwilini. Kuona hivyo, yule mtoto akawa hana jinsi. Huku akilia, akaanza kunywa kojo lake.
Wenzie wakaingiwa woga na kubaki wakikodoa macho. Wengine wakapiga kelele na kumuomba mwalimu wao asitishe adhabu hiyo, lakini haikusaidia.
Hatimaye, mwanafunzi yule wa kiume akanywa kojo lote na hapo mwalimu akamruhusu akakae, huku akiwataka wengine wasisimulie kokote jambo hilo.
Hata hivyo, licha ya mwalimu kuwachimba mkwara kuwa wasiseme kokote, baadhi ya wanafunzi walihadithia unyama huo majumbani kwao, akiwemo yule aliyekunywa mkojo.
Baada ya kusikia unyama huo, baadhi ya wazazi wakaja juu na kwenda kulalamika shuleni.
``Iliniuma sana. Nilitaka kwenda kushitaki polisi… lakini shuleni hapo wakaniomba niache na badala yake, uongozi wa shule ukasema utamuadhibu mwalimu kwa kosa hilo,`` mzazi wa mtoto huyo aliliambia Alasiri.
Hata hivyo, baadhi ya wazazi wamesema hawatakubali kuona suala hilo likimalizwa kienyeji.
``Mwalimu wa aina hii hafai, anaharibu sifa nzuri ya walimu wengine,`` akasema mzazi mmojawapo.
Alasiri bado inafuatilia sakata hilo kujua uongozi wa shule hiyo umechukua hatua gani.
|