|
Waziri Magufuli azungumzia matapeli wizarani kwake
2007-04-24 17:33:17
Na Frank Mbunda, Jijini
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. John Magufuli, amewataka wananchi wawe macho na matapeli wanaojifanya ni maofisa wa wizara hiyo wanaohusika na utoaji wa ofa, hati za viwanja na nyumba.
Waziri Magufuli amesema kuna makundi ya watu watanashati na wanaovalia suti kalikali huku wakijiweka jirani na jengo la wizara hiyo kwa ajili ya kuwaibia watu wasio na tahadhari ya kutosha dhidi yao, hasa wale wanaofika wizarani kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
``Ni vyema wananachi wakawa macho na watu hawa. Wanawachukulia fedha wananachi kwa gia ya kuwapa vibali vya ujenzi wa nyumba, hati za viwanja na mambo mengine… wawe makini ili wasitapeliwe,`` amesema Bw. Magufuli, aliyekuwa akizungumza katika kipindi cha Kipima Joto kilichorushwa na kituo cha Televisheni cha ITV Dar es Salaam.
Hatahivyo, Waziri Magufuli amesema tayari ameshawasiliana na polisi ili kuwasaka watu hao na kuwakamata ili waache kuibia wananachi.
Vilevile, Waziri Magufuli amesema hivi sasa wanafanya uchunguzi ili kubaini kama kuna baadhi ya maofisa wanaoshirikiana na matapeli hao.
``Hatutaki madalali wa kuuza ama kutoa hati za viwanja na nyumba katika wizara ya Ardhi, tunajua kuwapo kwao ni hatari,`` amesema Waziri Magufuli.
|