|
Kanumba alizwa, atimkia polisi
2007-04-24 17:35:38
Na Sharon Sauwa, Jijini
Muigizaji maarufu nchini na ambaye alitamba sana wakati akiigiza katika kituo cha luninga cha ITV, Stephen Kanumba, amelizwa vibaya na wajanja tele waliopo ndani ya Jiji hili na kulazimika kukimbilia polisi ili kupata msaada.
Msanii huyo ambaye awali alikuwa akitamba ITV na kundi la Kaole kabla hajajingea jina kupitia filamu alizoshirikiana na Wanigeria hivi karibuni, amejikuta akilizwa na wajanja wanaodurufu kazi za wasanii nchini na kuziuza kwa bei poa.
Kwa sababu ya kulizwa huko, Kanumba na Muimbaji wa nyimbo za dini , Bi. Jenifer Mgendi wameripoti katika kituo cha polisi Chan\'gombe na hadi sasa, watu wawili wamedakwa jana wakituhumiwa kudurufu kazi za wasanii bila idhini na kuziuza kwa bei poa.
Mgendi, ameiambia Alasiri kuwa kwa msaada wa polisi. Watu hao walidakwa jana jioni, ambao majina yao ni Said Hussein na Salum Seif.
Akasema kanda hizo zimekuwa zikiuzwa kwa Sh. 2,500 kwa jumla jumla wakati rejareja zinauzwa kwa Sh. 3,000 mpaka Sh. 3,500.
Akasema aliamua kwenda kuweka mtego katika maeneo ambayo walimwambia kanda hizo zinauzwa na kufanikiwa kuwakamata wamachinga hao ambao waliwapeleka wanapozinunua.
Akasema watu hao waliwapeleka katika chumba kimoja kilichopo eneo la Yombo ambapo waliwakamata watu hao wakiwa na kanda hizo pamoja na za wasanii wengine kibao.
Naye Stephen Kanumba akasema operesheni hiyo ilianza jana, ambapo wamegundua kanda hizo hudurufiwa majalada katika maeneo ya Ubungo na Temeke.
``Bado tunaendelea na operesheni hii...hawa wanakuwa wajanja wanavizia wanapoona mtu ametoa kanda ya video ama DVD au VCD wanakwenda kufanyia Scan na kuingiza sokoni kupitia wamachinga kabla ya wewe kuanza kuiuza,``akasema.
Kamanda wa mkoa wa kipolisi wa Temeke, Emmanuel Kandihabi amesema hadi sasa hajapelekewa taarifa rasmi kuhusiana na tukio hilo na akaahidi kuwa atalifuatilia.
|