26 Apr 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wakazi Temeke kuichongea manispaa kwa Kandoro
 
2007-04-26 17:00:49
Na Frank Mbunda, Mwembe Yanga

Zaidi ya wakazi 500 wa Mwemberadu, Kata ya Sandali iliyopo katika manispaa ya Temeke, wametishia kuandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakitaka kuondolewa kwa dampo lililo jirani na makazi yao.

Hatua ya wakazi hao inalenga katika kuishishinikiza Manispaa ya Temeke kusimamia zoezi la kulihamisha dampo hilo ambalo wamedai kwamba hivi sasa, linahatarisha afya zao, hasa watoto ambao muda mwingi huwa hapo wakicheza.

Baadhi ya wakazi hao wameiambia Alasiri juzi kuwa wataandamana kwenda kwa Bw. Kandoro kutokana na ukweli kuwa hivi sasa, wanapata shida kutokana na harufu mbaya ya taka zilizofurika katika eneo hilo.

Wakizungumza na Alasiri, baadhi ya wakazi hao wamesema awali eneo hilo la uwanja hakukuwa na dampo, bali kizimba kilichotumika kuhifadhi taka kwa muda kabla baadaye kutelekezwa na kuwa kama dampo.

``Manispaa imekuwa ikiahidi kuliondoa dampo hili mara kadhaa sasa… lakini utekelezaji wa ahadi hizo hauonekani na kwa sababu hiyo, tunafikiria kuandamana kwa Mkuu wa Mkoa ili kilio chetu kisikilizwe na kufanyiwa kazi,`` akasema Bw. Amani Mushi, mmoja wa wakazi hao.

Bw. Mushi akasema kuwapo kwa dampo katika eneo hilo lenye uwanja wa mikutano, michezo na bustani, kunasababisha matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza ari ya vijana kushiriki katika michezo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwemberadu, Bw. Mungi Mbwelezeni, amekiri kuwepo na malalamiko mengi kuhusiana na jalala hilo.

Akasema baadhi ya wananachi wenzie walishamtega kwa kutaka asimamie maandamano yao ya kwenda kwa mkuu wa mkoa, lakini amewaomba wawe wavumilivu ili awasiliane kwanza na Diwani wa Kata hiyo, Bw. Wilberd Tarimo.

``Nimewaomba wafanye subira kidogo, ili niweze kuwasiliana na diwani,`` akasema Bw. Mungi.

Alipoulizwa, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bw. Nyundo, amekiri kupokea malalamiko ya wakazi hao.

``Ni kweli, nimepokea madai hayo...ninawaomba wakazi wa eneo hilo wafanye subira na dampo hilo tutaliondoa wakati wowote kuanzia sasa kwa sababu kilichokuwa kikituchelewesha, ni eneo ambalo hivi sasa tumeshalipata,``akasema Bw. Nyundo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.