|
Shule ya Mwendapole Kibaha yawaasa `madenti` wake waliochaguliwa Sekondari
2007-04-30 15:50:22
Na Jacqueline Mosha, Kibaha
Wahitimu wa Shule ya Msingi Mwendapole iliyoko Wilayani Kibaha mkoa wa Pwani na kuchaguliwa kujiunga na shule mbalimbali za sekondari nchini, wametakiwa kutokuwa na tamaa na badala yake kusoma na kuelewa kuliko kukariri.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Mwajuma Tyeah, ametoa wito huo wiki hii shuleni hapo, wakati akisoma risala fupi katika sherehe ya kuwapongeza wanafunzi waliochaguliwa sekondari na pia kuwashukuru wazazi wao kwa mwongozo na ushirikiano mzuri walioonyesha kwa watoto wao hadi wakafaulu.
Bi. Tyeah, akasema wanafunzi waliohitimu na kupata nafasi ya kuendelea na sekondari, wanapaswa kuongeza juhudi na kujituma zaidi kwani masomo ya sekondari yanafundishwa kwa upana na yanahitaji uelewa kuliko kukariri.
``Jamani elimu ya sekondari si ya lelemama, inahitaji kuwa na bidii ya kusoma na kuelewa vizuri masomo yenu, msidhani kwamba huko kuna kukariri, hapana, soma uelewe na panapokushinda usisite kumuuliza mwalimu wa somo, msione aibu huko,`` akasisitiza Bi. Tyeah.
Kadhalika Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo Bi. Subira Komba, akawaasa wanafunzi hao kutokuzichezea nafasi walizozipata kwa kuwa makini na kuzikwepa tamaa na vishawishi vitakavyowasababishia kuacha shule na kuwapa hasara wazazi wao.
``Msichezee nafasi hizo ni za muhimu kwa maisha yenu na ya wazazi wenu, ni tunu ambayo mkiichezea vibaya mtajutia baadaye, huo ndio urithi mliopata toka kwa walimu na wazazi hivyo someni kwa nguvu zenu zote mpaka mfike vyuo vikuu na kupata kazi nzuri,`` Mwalimu Komba akawaambia wanafunzi hao.
Hata hivyo wazazi na wanafunzi waliochaguliwa wakaushukuru uongozi wa shule hiyo na kamati yake kwa jitihada zilizopelekea watoto kufaulu kwa kiwango hicho. Pia wakawapa pole wanafunzi wanne waliokosa nafasi za kuchaguliwa.
Mwaka jana, shule hiyo iliyopo kwenye mpango wa usomaji vitabu kwa watoto nchini, CBP, ilipata ushindi wa kwanza baada ya kuongoza kwa huduma bora za maktaba, zana za kufundishia za ubunifu, kuchora na utambuzi juu ya ukimwi na kukabidhiwa kombe, ngao kuu na vyeti vitano.
Shule hiyo ina maktaba yenye uwezo wa kuingia wanafunzi 40 kwa siku huku zaidi ya wanafunzi na watu 500 wanaoishi jirani na shule hiyo hufika kujisomea vitabu mbalimbali kila mwezi.
|