|
Waziri Simba kuchangisha fedha za bweni la wasichana Loyola
2007-04-30 15:51:31
Na Usu-Emma Sindila, Jijini
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Sofia Simba, anatarajiwa kuongoza harambee ya kuchangia fedha za ujenzi wa mabweni ya wasichana katika Shule ya Sekondari Loyola Jijini.
Harambee hiyo, inayotarajiwa kuingiza fedha zitakazosaidia kupatikana kwa Sh. Milioni 230 zinazohitajika kwa ujenzi huo, itafanyika Mei Mosi, kuanzia mishale ya saa 12:00 jioni hadi saa 4:00 usiku katika ukumbi wa shule hiyo iliyopo Mabibo Jijini.
Mkuu wa shule hiyo, Father Manyahi, amesema shule yake inahitaji Sh. Milioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wasichana ambapo kiasi cha fedha kitakachopatikana katika chakula cha jioni siku hiyo, kitatumika kwa ajili ya ujenzi huo.
Wakizungumza na waaandishi wa habari Jijini, wanafunzi wa shule hiyo waliosindikizwa na Mkuu wa shule hiyo, Father Jerome Manyahi, wamesema ujenzi huo utarahisisha makazi kwa wanafunzi hao wanaopata shida ya usafiri wa jiji hili.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi hao, Anna Sanga mwanafunzi wa kidato cha sita amesema, wanafunzi wa kike wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la vishawishi vingi barabarani tangu wanapoanza safari ya nyumbani kwenda shule na kutoka shule kwenda nyumbani.
Amesema licha ya vishawishi hivyo wanafunzi wa kike wamekuwa wakikabiliwa na shida ya usafiri unaosababishwa na baadhi ya madereva na makondakta wa daladala, pamoja na lugha chafu zinazotolewa na wahudumu hao.
``Wanafunzi wanapoteza muda mwingi wakiwa njia, na wasichana wanaporudi majumbani wanakumbana na kazi za nyumbani tena, wanapomaliza wanakuwa wamechoka na hawawezi tena kusoma na kujiandaa na masomo ya siku inayofuata,`` akasema Anna.
Naye mwanafunzi mwingine, Jenipher Mshamma, amesema ujenzi wa hosteli hiyo utamsaidia msichana kupata mwamko wa kusoma akiwa na wenzake tofauti na anavyokuwa peke yake nyumbani.
``Pia itamsaidia mtoto wa kike kuepuka kupoteza muda mwingi wa kusafiri kwama anakaa mbali na shule, hivyo atapata muda wa kupumzika na kujisomea zaidi,`` akasema.
Mwaka 2005, shule hiyo ilifanya matembezi ya hisani yaliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambapo kiasi cha milioni 30 zilipatikana na zimekwishatumika katika ujenzi wa awali wa jengo hilo.
Amesema pindi jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 60 kwa wakati mmoja, na kuongeza kuwa nia ya shule hiyo ni kujenga jengo litakalochukua zaidi ya wanafunzi 200.
|