|
Wafanyabiashara K`ndoni wachimbana `mkwara`
2007-04-30 15:53:39
Na Valery Kiyungu
Wafanyabiashara wanaoendelea kufanyia bioashara zao vichochoroni katika Manispaa ya Kinondoni Jijini, wametakiwa kuondoka maeneo hayo na kuhamia kwenye masoko waliyopangiwa.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Muungano wa Masoko Dar es Salaam,MUMADA, Kanda ya Kinondoni, Bw. Mohammed Mwenkya, wakati akizungumza katika mkutano wa wafanyabishara uliofanyika Tandale Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umekutanisha wafanyabiashara wa masoko ya Mbezi Juu, Mkunguni, Mabibo, Msasani na Kunduchi Jijini.
Bw. Mwekya amewapa muda wa mwezi mmoja wafanyabiashara hao kuhamia kwenye masoko hayo kabla hatua zaidi hazijachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha askari wa kubomoa vibanda vyao.
``MUMADA inawapa mwezi mmoja wachuuzi wanaofanya shughuli zao kwenye magenge katika Manispaa ya Kinondoni kuhamia katika masoko waliyoelekezwa,``amesema Bw. Mwenkya.
Amesema kuwa ofisi yake imepata malalamiko kutoka kwa wachuuzi wa masoko hayo kwamba wenzao,wanaendeshea shughuli zao kwenye magenge licha ya kuelekezwa kuhamia katika maeneo maalumu yaliyotengwa na Manispaa.
Amesema kuwa kitendo cha wafanyabiashara kung’ang’ania kuendesha shughuli zao maeneo hayo walikataliwa kinawanyima wateja wenzao walioko kwenye masoko yalipangwa.
Amesema kwa utaratibu mpya wa Jiji, wenye magenge eneo la Mbezi Beach, wanatakiwa kuhamia katika soko la Mbezi Juu wakati wale walioko magenge ya Hananasif, wameelekezwa kuhamia katika soko la Mkunguni.
Akasisisiza kuwa wafanyabiashara wanaoendeshea shughuli zao eneo la Makutano, watakiwa kwenda kujiunga katika soko la Mabibo na wale eneo la Msasani wanatakiwa kuhamia kwenye soko la Bonde la Mpunga.
Pia akasema kuwa masoko yaliyoko Kunduchi yanelazimika kuhamishiwa soko la Nyuki Tegeta.
Awali uongozi wa MUMADA,umewahi kutoa siku 21 kwa wafanyabiashara waliokimbia meza zao katika masoko matatu ya Mburahati NHC, Manzese na Mabibo kurejea mara moja kabla nafasi zao hawajapewa watu wengine.
Mwenyekiti huyo,amewakumbusha wafanyabiashara wa masoko ambao wamekimbia kujua kwamba nafasi zao watazipoteza endapo watashindwa kutekeleza agizo hilo ndani ya kipindi hicho cha siku 21.
|