|
Mei Mosi kesho Mambo safiiii!
2007-04-30 15:54:49
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Kodi nchini, TRA na nia ya dhati ya Serikali ya awamu ya nne katika kuboresha maslahi ya watumishi wake, ni baadhi ya mambo yanayoashiria kwamba kesho, wafanyakazi nchini watapata furaha ya aina yake katika kusherehekea Sikukuu yao ya Mei Mosi kwa Serikali kuwatangazia mambo safiiii!
Kwa mujibu wa taarifa za makusanyo ya TRA, inaonyesha kuwa hivi sasa, Mamlaka hiyo iliyo makini zaidi katika kutimiza malengo yake, inatunisha mfuko wa Serikali ipasavyo kwa kuingiizia zaidi ya Sh. Bilioni 260 kwa mwezi na hivyo kutoa matumaini mapya kwa wafanyakazi hiyo kesho.
Lakini, mbali na TRA, pia Rais Kikwete alishaahidi mara kadhaa kuwa Serikali yake imekusudia kuboresha hali za wafanyakazi ambapo katika kufikia azma hiyo, akaunda tume ambayo imeripotiwa kuwa tayari imeshamaliza kazi yake na kumkabidhi ripoti.
Kwa sababu hiyo, Sherehe za Mei Mosi ambazo husherehekewa na wafanyakazi duniani kote, zinatarajiwa kuwa ‘bomba’ zaidi kwa wafanyakazi nchini.
Walimu, wauguzi, madaktari, askari na watumishi wengine wa umma, wanatarajiwa kutangaziwa donge nono la mishahara na malupulupu mapya ambayo msingi wake, ni ahadi hiyo ya Rais Kikwete na Serikali yake ya awamu ya nne katika kuboresha hali za wafanyakazi katika kila bajeti na kadiri hali ya uchumi inavyoimarika.
Juzi, akizungumza katika ufunguzi rasmi wa Jengo la Walimu pale Ilala Jijini, `Mwalimu House`, Rais Kikwete alitangaza kwamba, kwa kutambua umuhimu wa kazi zao kwa taifa, Serikali itawaongezea mishahara walimu na watumishi wengine wa Serikali katika bajeti yake ijayo.
Akasema ni nia ya Serikali katika kuwafanya watumishi wake wawe na hali bora na kwa sababu hiyo, itawaongezea mishahara na pia kuendelea na zoezi hilo la uboreshaji kadri hali ya mapato ya serikali inavyozidi kuwa nzuri.
Kwa sababu hizo, wafuatiliaji wa mambo wanasema kesho kwenye Mei Mosi, wafanyakazi watasherehekea kwa furaha zaidi kwa matumaini ya kutangaziwa rasmi nyongeza ya mishahara na vivutio vingine kadhaa vya kuwafanya waongeze ufanisi katika majukumu yao.
|