|
Majani ya mifugo yanalipa
2007-06-12 16:24:15
Na Aziz Issa
Kuporomoka kwa bei ya kahawa kumesababisha wakulima wilayani Same kuliweka kando zao hilo na kuanzisha kilimo cha majani ya kulishia mifugo.
Wanachama wa kikundi cha ufufuaji wa zao la Kahawa bora wa kijiji cha Foo, Kiufoo, kilichopo wilayani Same waliwaambia hayo waandihi wa habari waliokitembelea kikundi hicho kuangalia sababu zinazochangia kuzorotesha maendeleo ya uzalishaji wa kahawa.
Wanakikundi hao walisema wakulima wa kahawa wamefikia uamuzi huo wa kulima majani ya kulishia mifugo, baada ya kuona gharama za uzalishaji wa zao hilo zikiwa juu huku bei yake ikizidi kuporomoka.
Mwenyekiti wa kikundi hicho Bw. Peter Mushi alisema uzalishaji wa kahawa unaporomoka kutokana na baadhi ya wakulima kuamua kukata kahawa na kupanda majani, huku wengine wakiyatelekeza mashamba yao kuwa mapori.
Akasema wakulima hao wamekuwa wakilima majani aina ya Gwatemala, Elephatiki na Stereo na kwamba katika ekari moja ya majani hayo huwaingizia Shilingi 700,000 hadi Milioni moja kwa mwaka.
Akasema pia kuna baadhi ya wakulima wamekuwa waking`oa mikahawa na kupanda mazao ya muda mfupi kama vile mahindi, maharage, nyanya, karoti na kabichi, mazao yanayowaletea pesa nyingi kuliko kahawa kwa sasa.
|