12 Jun 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Samaki wa ajabu avuliwa Jijini Dar
 
2007-06-12 16:31:53
Na Emmanuel Lengwa, Feri

Samaki mwenye urefu wa mita moja na nusu na uzito wa kilo 74 amevuliwa katika pwani ya Dar es Salaam huku waliohusika katika uvuajhi wa samaki huyo wakijihisi kuingizwa mjini baada ya kudai kuwa watu wa manispaa wamemchukua bila kuwapa hata senti tano kutokana na kazi yao ya kumnasa samaki huyo na kumfikisha pale kwenye Soko la Samaki la kimataifa, Feri.

Mkuu wa soko la samaki la Kimataifa la Feri, Bw. Walter Macha, amesema samaki huyo alifikishwa sokoni hapo juzi, mishale ya saa 7:00 mchana.

`Wavuvi watano ambao ni wenyeji wa kisiwa cha Unguja ndio waliomvua samaki huyo wakiwa na chombo chao chenye namba WMAU 1511. Kama walivyo wavuvi wengine, walimleta sokoni kwetu ili kumuuza,`akasema Bw. Macha.

Akawataja wavuvi waliomnasa samaki huyo kuwa ni pamoja na Bw. Simai Ami Simai, Yusuph Mzee, Kibabu Daniel na Bakari Ali Mfaume, wote wakazi wa Unguja.

Akasema baada ya kuona watu wengi, wakiwamo wavuvi wakongwe wakishangaa na kushindwa kumtambua samaki huyo, ndipo walipoamua kuwasiliana na kitengo cha utafiti wa Samaki, TAFIRI na kuwajulisha kuwapo kwa samaki huyo.

`Tulipowajulisha watu wa TAFIRI wakaagiza tumuhifadhi mpaka watakapokuja kumchunguza zaidi,` akasema Bw. Macha.

Akizungumza na Alasiri, mmoja wa wavuvi hao, Bw. Simai, amesema samaki huyo walimvua katika kisiwa cha Sinda kilicho jirani na maeneo ambayo hutumika zinapopaki meli zinazosubiri kuingia Bandari ya Dar es Salaam, umbali wa kama kilometa tano hivi kutoka lilipo soko la Feri.

Amesema waliweza kumvua samaki huyo kwa kutumia nyavu zinazotumika kuvulia samaki aina ya papa.

Akasema walitandaza nyavu zao Juni 8, mishale ya saa 8:00 mchana na kesho yake saa 2:00 asubuhi walipokwenda kuzitoa, wakamkuta samaki huyo na wengine kadhaa.

Bw. Simai akasema walipoona wamevua samaki wengi wakaamua kuwaleta katika soko la Feri kuwauza.

`Tuliwauza samaki wengine wote kasoro huyu ambaye hatambuliki jina... kabla hatujaamua cha kufanya, wakaja watu wa Manispaa na kutuomba tuwapatie,` akasema Bw. Simai.

Hata hivyo, Bw. Simai anasema licha ya samaki huyo kushikiliwa na uongozi wa soko hilo, bado hawajalipwa chochote na wala hawajui hatma ya samaki huyo wa ajabu.

`Mpaka sasa hatujui kama samaki huyu ni mali yetu au ni wa Maliasili. Na hadi sasa tunapoongea, hakuna tulichopewa kwa kazi yetu ya kumvua na kumsafirisha hadi hapa,` akasema Bw. Simai.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii, wavuvi mbalimbali sokoni hapo wamesema wameshindwa kujua jina la samaki huyo, ingawa baadhi wamekuwa wakimfananisha na samaki mwingine aitwaye Chewa.

Mkuu wa soko hilo amesema hata wao wanasubiri uchunguzi wa wataalamu wa TAFIRI ambao ndio wanaweza kutoa maelezo juu ya samaki huyo.

`Nadhani TAFIRI ndio watatupatia maelezo zaidi ya samaki huyu. Naamini wao ni wataalamu zaidi wa mambo ya utafiti, hivyo wanaweza kujua jina, umri, kizazi na sifa zake nyingine nyingi,` akasema Mkuu huyo wa soko.

Mpaka Alasiri inaondoka sokoni hapo, wataalamu wa TAFIRI walikuwa bado hawajafika ili kueleza ya kwao kuhusiana na samaki huyo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.