|
Bar Jijini yavamiwa
2007-06-12 16:35:13
Na Job Ndomba, Mwenge
Kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi limevamia bar moja maarufu Jijini na kuua mtu mmoja kwa kumcharanga mapanga kabla ya kuingia mitini baada ya kufeli kwa jaribio lao la kupora mali.
Tukio hilo limetokea Mwenge usiku wa kuamkia leo, mishale ya saa 9:00, pale katika bar maarufu ya Maryland, wakati wanywaji wakiwa tayari wameshajiondokea makwao.
Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, mmoja wa walinzi wa eneo hilo, Bw. Sandles Mwansambo, amemtaja mtu aliyefariki kuwa ni mlinzi mwenzie aitwaye Lauriano Ubwalo, wa Kampuni ya Ulinzi ya BAKISA.
Akisimulia tukio hilo, Bw. Mwansambo amesema baada ya majambazi hayo kutinga maeneo hayo, walimtia kabali marehemu na kuanza kumpiga kwa nyundo, marungu na mapanga.
Akasema Bw. Mwansambo kuwa baada ya kumjeruhi vibaya na damu nyingi, majambazi hayo yalibaini kuwa yameshastukiwa na hivyo yakatimua mbio kutoka mahala hapo na kumuacha marehemu akiwa taabani.
Naye mfanyakazi mwingine wa Bar hiyo aitwaye Musa Mdesa, amesema mlinzi huyo alikuwa akilinda duka la nguo lililopo mahala hapo.
Naye mmiliki wa duka alilokuwa akilinda mlinzi huyo lijulikanalo kama Bosandra Proffessionals, Bi. Bora Haule, amesema marehemu alikuwa mlinzi wake na alipigiwa simu muda mfupi baada ya tukio hilo kutokea na ndipo akawajulisha Polisi kwa nia ya kuhitaji msaada wao.
Naye Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jamal Rwambow, amethibitisha kuwepo kwa uvamizi huo.
Hatahivyo akasema yeye hakuwa na taarifa za kifo cha mlinzi huyo na hivyo ameagiza vijana wake kwenda kuthibitisha pale katika Hospitali ya Mwananyamala.
|