|
Chungu ya mahaba
2007-06-12 16:36:05
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili
Wivu wa mapenzi umezua balaa zito lililopelekea wanaume wazima kutaka kutoana roho. Sasa mmoja wao yuko hoi bin taaban katika hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kuvunjwa shingo.
Sekesele lenyewe limefuatia jamaa mmoja, huku akiwa na hasira kama mbogo, kuwaangushia kipigo rafiki zake akiwatuhumu kula njama za kumtorosha mchumba wake.
Akizungumza na Alasiri wodini hapo mmoja wa wahanga wa tukio hilo, Shomari Salum, 25, amesema tukio hilo lilitokea majuzi saa 4:30 usiku, huko Shule ya msingi Tandale Magharibi, Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Shomari, rafiki yake mmoja aliyemtaja kwa jina la Frank ndiye aliyelianzisha baada ya kumtuhumu kuwa ni mmoja kati wa watu waliohusika katika tukio la kumtorosha mpenzi wake.
Akasema siku hiyo ya tukio, alikwenda kumtembelea rafiki yake huyo kwa ajili ya mazungumzo ya kawaida, alipofika huko akakutana na washikaji wao wengine na katika maongezi yao, Frank akawatuhumu kuwa wanafahamu dili zima la mchumba wake kutoweka na kwenda kuishi na mwanaume mwingine.
Akasema baada ya kuingiza mada hiyo, wote walipinga kuhusika na jambo hilo, hatua iliyomfanya Frank kupandwa na jazba na kuanza kuwashindilia makofi rafiki zake hao.
Kwa mujibu wa Shomai, Frank alimkamata (Shomari) na kumnyanyua mzobe mzobe na kumbwaga kwenye barabara ya lami, hali iliyosababisha avunjike shingo.
`Nilishtukia mwezangu akinikamata na kuniangusha juu ya lami, fahamu zilitoweka na sikujua kilichoendelea tena, hadi niliposhtuka nikiwa hapa Moi huku shingo yangu ikiwa imevunjika,` akasema Shomari.
Hata hivyo Shomari amepinga kuhusika kusambaratisha penzi la wawili hao, na kudai kuwa chanzo cha mchumba huyo kumkimbia rafiki yake ni tabia yake ya kugombana kila siku.
Akaongeza kuwa tabia hiyo ilimuudhi binti wa watu na kuamua kwenda kuishi na mwanaume mwingine ambaye anaishi nyumba moja na mmoja wa marafiki zao.
`Ni kweli mchumba wake kamkimbia, lakini sio sisi tuliosababisha ila yeye mwenyewe kwa mikono yake ndo aliyevunja uhusiano huo kutokana na tabia yake ya kugombana gombana,` akasema.
Naye, Kaimu Afisa Uhusiano wa Moi, Bi Mary Ocheng, amesema mgonjwa huyo alifikishwa hospitalini hapo majira ya saa 7:00 usiku, akiwa amepoteza fahamu na kukimbizwa wodini ili kupatiwa matibabu.
|