|
Majambazi Dar yamwagiwa risasi usiku
2007-06-15 16:20:28
Na Job Ndomba, Mwenge
Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamekurupushwa toka kwenye duka moja walilotaka kupora mali na kulazimika kutimua mbio huku wakitelekeza gari lao lililojaa michirizi ya damu.
Watu hao wamekurupushwa usiku wa kuamkia jana na polisi waliotaarifiwa mapema juu ya tukio hilo na kudaiwa kumchapa risasi mmoja wao.
Hatahivyo, inadaiwa kuwa jambazi aliyepigwa risasi aliweza kutimua mbio na wenzie licha ya kutokwa na damu nyingi.
Tukio hilo limejiri mishale ya saa 10.00 usiku wa kuamkia jana pale maeneo ya Mwenge Kijijini wakati majambazi hao walipokutwa wakihangaika kuvunja makufuli ya mlango wa duka la mfanyabiashara aitwaye Sekutule Mshack.
Imeelezwa kuwa polisi waliofanya kazi hiyo ni wale waliokuwa zamu katika lindo lao pale kwenye ofisi za Manispaa ya Kinodnoni za Mamlaka ya Kodi nchini, TRA, zilizopo Mwenge.
Inaelezwa kuwa baada ya askari hao kutaarifiwa juu ya uvamizi wa majmbazi hao waliokuwa na gari dogo, wakawanyatia kwa upole na mwishowe kuwakurupusha.
Kwa mujibu wa mlinzi mmoja wa Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate Security aliyekuwa jirani na eneo la tukio, ni kwamba majambazi hao walikuwa wanne.
Naye mmiliki wa duka hilo, Bw. Mshack, amesema mida hiyo, yeye alikuwa amelala usiku, lakini akaamka baada ya kusikia mirindimo ya risasi
Akasema anashukuru kuwa duka lake halikuibiwa chochote kutokana na kazi nzuri ya polisi.
Naye Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow, amesema yeye alikuwa bado hajapata taarifa kamili za tukio hilo.
Aidha Alasiri lilipofuatilia zaidi tukio hilo pale Kituo cha Polisi cha Mabatini, ililikuta gari linalohusishwa na tukio hilo kuwa ni T 627 AAK aina ya Toyota Corolla.
|