|
Mwanafunzi darasa la tano Dar auawa kinyama
2007-06-15 16:28:31
Na Mwanaidi Swedi, Jijini
Mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Bunju B, Bi. Rahma Abbas, 13, ameokotwa akiwa ameuwawa na watu wasiofahamika huku akiwa amefungwa kamba shingoni na mikononi.
Kamanda wa mkoa wa kipolisi Kinondoni, Jamal Rwambow, amesema tukio hilo limetokea juzi, mishale ya saa 1:00 asubuhi huko Bunju B Jijini, karibu na nyumba ya bwana mmoja aitwaye Jumanne Mohamed.
Kamanda Rwambow amesema sababu ya kuuawa kwa mwanafunzo huyo hazijaweza kufahamika mara moja na hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Mwananyamala.
Wakati huohuo, watu saba wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na kilo nane za bangi, misokoto 400 ya bangi na lita 65 za pombe haramu ya gongo.
Kamanda Rwambow amesema tukio hilo limetokea juzi huko Kimara Kibo na Kimara Suca Jijini, mishale ya saa 8:00 mchana baada ya askari polisi kufanya msako.
Akasema Kamanda Rwambow kuwa watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
|