|
Majambazi tena: Risasi zatembea, gari lajaa damu
2007-06-15 16:30:38
Na Job Ndomba, Mwenge
Wakati Jeshi la Polisi likiendelea kula nao sahani moja, majambazi Jijini Dar wameendelea kusumbua katika baadhi ya maeneo ambapo juzi usiku wamevamia duka moja kwa nia ya kukomba mali zilizokuwamo.
Tukio hilo linaloashiria kwamba vita dhidi yao bado mbichi, limejiri pale Mwenge Kijijini usiku wa kuamkia jana ambapo hatahivyo, jambazi mmoja alijikuta akilimwa risasi na gari lao kunaswa huku likiwa na `midamu` kibao.
Majambazi hao wamekurupushwa katika na polisi waliotaarifiwa mapema juu ya tukio hilo lililoambatana na kutembeazeana risasi.
Hatahivyo, inadaiwa kuwa jambazi aliyepigwa risasi aliweza kutimua mbio na wenzie licha ya kutokwa na damu nyingi.
Tukio hilo limejiri mishale ya saa 10.00 usiku wakati majambazi hao walipokutwa wakihangaika kuvunja makufuli ya mlango wa duka la mfanyabiashara aitwaye Sekutule Mshack.
Imeelezwa kuwa polisi waliofanya kazi hiyo ni wale waliokuwa zamu katika lindo lao la Ofisi za Mamlka ya Mapato Nchini, TRA, zilizopo Mwenge.
Inaelezwa kuwa baada ya askari hao kutaarifiwa juu ya uvamizi wa majmbazi hao waliokuwa na gari dogo, wakawanyatia kwa upole na mwishowe kuwakurupusha.
Kwa mujibu wa mlinzi mmoja wa Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate Security aliyekuwa jirani na eneo la tukio, ni kwamba majambazi hao walikuwa wanne.
Naye mmiliki wa duka hilo, Bw. Mshack, amesema mida hiyo, yeye alikuwa amelala usiku, lakini akaamka baada ya kusikia mirindimo ya risasi.
Akasema anashukuru kuwa duka lake halikuibiwa chochote kutokana na kazi nzuri ya polisi.
Aidha, Alasiri lilipofuatilia zaidi tukio hilo pale katika Kituo cha Polisi Kijitonyama Mabatini, ililikuta gari linalodaiwa kuhusika na na tukio hilo, Toyota Corolla lenye namba T 627 AAK.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jamal Rwambow, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa hadi sasa, vijana wake wanaendelea na upelelezi mkali juu ya kile kilichojiri.
|