|
Wabunge wapinzani waiponda bajeti
2007-06-15 16:33:42
Na Kiyao Hoza, Dodoma
Baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani nchini, wameiponda vikali bajeti ya mwaka mpya wa fedha wa 2007/2008 iliyowasilishwa jana mjini hapa na Waziri wa Fedha Bi. Zakia Meghji.
Wakizungumza na Alasiri kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamesema bajeti hiyo ni mzigo kwa Mtanzania wa kawaida.
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), Bw. John Cheyo almaarufu kama Bw. Mapesa amesema ingawa bajeti hiyo inaonyesha kuwa Serikali inakusudia kuwasaidia wananchi wake, lakini anaamini imejaa kiini macho kwa vile Serikali hiyohiyo inakabiliwa na ukata nkubwa wa pesa.
Akasema kwa sababu hiyo, anaamini Serikali itaendelea kuwakamua wananchi wake kwa kisingizio cha kukusanya michango ya ujenzi wa shule, zahanati, barabara, maji na huduma nyinginezo ambazo yenyewe inapaswa kuzitoa kwa wananchi wake.
Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, amesema bajeti hiyo bado hailengi kuleta maisha bora kwa Mtanzania wa kawaida na badala yake inanufaisha wenye nacho.
`Serikali ni lazima ijue kuwa wale wanywaji wa bia, hivi sasa wanaweza kuhamia kwenye gongo ili kukwepa gharama. Na hili ni tatizo jingine kubwa,` akasema Dk. Slaa ambaye pia ameponda upandishwaji wa kodi ya mafuta.
Pia amesema upo uwezekanao wa nauli katika huduma ya usafiri, kama daladala na taksi kuongezeka, kwa vile kodi ya mafuta ya petroli na dizeli pia imeongezeka.
Pamoja na wabunge hao kuikosoa bajeti hiyo, hali ya waheshimiwa wabunge kutokubaliana na bajeti hiyo, ilijitokeza wakati Waziri Meghji akiwasilisha bajeti yake, ambapo ilikuwa ikizuka minong\'ono iliyomlazimu Spika kuingilia kati.
|