|
Kitita kipya mwezi ujao
2007-06-15 16:34:52
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Baada ya ile tume ya Rais kuhusiana na namna ya kuboresha maslahi ya watumishi wa Serikali kukabidhi mapendekezo yake, hatimaye mambo yameanza kuwa `supa` baada ya kuelezwa kuwa kitita kipya kitaanza kutua mikononi mwa wahusika siku si nyingi.
Kulingana na hotuba ya bajeti iliyosomwa Bungeni jana na Waziri wa Fedha, Bi. Zakia Meghji, huenda kitita kipya kitaanza kutolewa mwezi ujao.
Ingawa Waziri hakusema wazi kuwa mishahara mipya itaanza mwezi ujao lakini alitangaza kwamba Serikali inaanza kufanyia kazi mapendekezo hayo kwa awamu.
Alisema Waziri wa Utumishi, Bi. Hawa Ghasia, atazungumzia kwa kina juu ya mabadiliko ya mishahara wakati wa kusoma bajeti ya wizara yake na hivyo mishahara hiyo mipya.
Aidha, katika kuahirisha kikao cha bunge jana, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Samwel Sitta, alisema atahakikisha Waziri wa Utumishi anapata nafasi ya kuwasilisha bajeti yake mapema ili watu wajue kuhusu kilichobadilika katika msihahara yao.
Pia Waziri Meghji alitangaza kuhusu kupunguzwa kwa kiwango cha kodi katika mishahara ambapo ule wa kima cha chini, sasa utakatwa kwa asilimia 15, badala ya 18.5 za awali, hivyo kumhakikishia mfanyakazi mshahara mnono zaidi.
|