15 Jun 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wanao twafwaa!
 
2007-06-15 16:37:09
Na Mwandishi Wetu, Jijini

Kutangazwa kwa ongezeko la kodi ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa katika bajeti iliyotangazwa jana na Waziri wa Fedha Bi. Zakia Meghji kumetajwa kuwa ni pigo kubwa kwa wenye kipato cha chini na tayari baadhi yao wameanza kuingiwa hofu wakidai kuwa sasa wafwa!

Wakizungumza na Alasiri kwa nyakati tofauti kuhusiana na bajeti iliyotangazwa jana na Serikali, baadhi ya wakazi wa Jijini wamesema ongezeko la ushuru wa mafuta ya petroli kwa mfano, kutoka Sh.100 kwa lita hadi Sh. 200, kutafanya vitu vingi muhimu kupanda.

Wakasema kwa sababu mafuta ndiyo muhimili wa biashara zote, kupanda kwake kutasababisha bidhaa zote kupanda bei na matokeo yake, watu wa kipato cha chini ndio watakaoumia zaidi na kuwafanya waondokane kabisa na ndoto ya siku moja kuwa na `maisha bora`.

Bi.Salma Bakari, mkazi wa Tandika ambaye hukaanga samaki na kuwauza, amesema kupanda kwa mafuta kunatishia nauli za daladala ambazo kwa vyovyote vile zitapanda maradufu na pia bidhaa kama unga na mchele zitapanda zaidi.

`Sielewi kama wanataka kutuua kijanja au vipi… hivi sasa, mimi na wanangu watatu tunataabika kupata milo miwili kwa siku. Sasa bei za vyakula zikiongezeka sijui hali itakuwaje,` akasema Bi. Salma.

Naye mfanyabiashara ya viatu pale Manzese, Bw. Paul Jacob, amesema anashangaa kuona siku zote bajeti zimekuwa hazioi matumaini kwa watu wa chini kama yeye.

`Mimi kwa kweli nimekata tamaa kabisa. Bajeti hii itaniwia vigumu katika kutimiza ndoto zangu za kujikwamua na umaskini… naamini kila nitakachopata kitaishia kwenye usafiri na tumboni, basi.`

Naye Mwenyekiti wa chama cha TLP, Bw. Agustino Mrema amekuja juu kuhusiana na kupanda kwa mafuta na ameungana na wananchi kudai kuwa imekuwa ya kikandamizaji.

Bw. Mrema amesema kupanda kwa bei ya mafuta kunaendelea kumpa mzigo mzito mkulima ambaye atashindwa kusafirisha hata kile kidogo anachozalisha sasa.

Amesema bei ya mafuta ikiwa juu itaendelea kulifanya taifa kuwa ombaomba na kwamba falsafa ya maisha bora kwa kilia Mtanzania itakuwa kiini macho.

`Hii bajeti bwana imezidi kumkandamiza yule mwananchi wa kijijini, kwani mafuta yakiwa bei juu ni lazima maisha kwa ujumla yatapanda na hivyo mtu huyo atashindwa kujimudu,`akasema.

Aidha amesema kupanda kwa bei ya mafuta kutaathiri sekta nyingi zikiwemo za uzalishaji na zile za elimu kwani watu watashindwa hata kuwalipia nauli watoto wao.

Jana waziri wa Fedha Bi. Zakhia Megji alisoma bajeti ya Serikali ya mwaka 2007/2008 na katika bajeti yake imeonyesha moja ya vitu vinavyoashiria kuwatesa wananchi ni kupanda kwa bei ya mafuta.

Wakati huohuo Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu, SUMATRA, imesema imeshtushwa sana na uamuzi wa Serikali kupandisha kodi ya mafuta.

Akiongea na gazeti hili leo asubuhi, Meneja Mawasiliano ya Umma wa taasisi hiyo, Bw. David Mziray amesema Sumatra imestushwa na uamuzi wa Serikali kupandisha kodi ya mafuta.

Amesema hivi sasa hatma ya wananchi wa kawaida iko mikononi mwa waheshimiwa wabunge ambao ndio wanayo dhamana ya kutetea maslahi ya wananchi bungeni.

Akasema ikiwa mambo yatabaki kama yalivyotangazwa jana, itabidi SUMATRA ikae chini na wadau wa usafirishaji ili kuona uwezekano wa kuendesha shughuli za usafishaji, bila kuumiza upande mmoja.

`Bajeti hiyo imesomwa jana, tusubiri mpaka mwisho tuone wabunge watatoa hoja gani za kuishawishi Serikali ipunguze kodi ya mafuta, lakini ikiwa itabaki kama ilivyo, itabidi mwezi Julai tukae na wadau kujadili namna ya kufanya, maana sisi SUMATRA tunaendesha kazi zetu kwa kutumia mbinu shirikishi,` akasema Bw. Mziray.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.