|
Mrembo asakwa akidaiwa kukomba mapesa ya hoteli
2007-06-16 18:28:08
Na Adam Fungamwango, Boko
Mtunza fedha wa hoteli ya Boko Inn Jijini Dar es Salaam, Bi. Norin Hassan, 22, anasakwa kwa udi na uvumba akidaiwa kuingia mitini na mamilioni ya pesa za mishahara ya wafanyakazi wa hoteli hiyo ikiwa ni muda mfupi tu kabla ya kuwalipa.
Mtunza fedha huyo anadaiwa kupewa pesa hizo ili awalipe mishahara wafanyakazi wote wa hoteli hiyo, baada ya muda mfupi aliomba udhuru na kuahidi angerejea baadaye na hadi leo hajaonekana.
Akizungumza na Alasiri, Meneja wa hoteli hiyo iliyopo nje kidogo ya Jiji, Bw. Godbles Masaoe, amedai kuwa mbali na mishahara ya wafanyakazi, pia mtunza fedha huyo ameondoka na pesa za mauzo ya wiki mbili.
`Kwa sasa kiasi kamili cha pesa alichoondoka nacho bado hakijajulikana… mpaka tutakapokaa chini na kupiga mahesabu ya mishahara hiyo na kujumlisha na pesa za mauzo ya hoteli ndipo hapo tutakapopata kiasi cha pesa alichokimbia nacho, lakini ni mapesa mengi,`akasema meneja huyo.
Bw. Masaoe akadai kuwa tukio hilo lilitokea Juni 2 mwaka huu ambapo baada ya kukabidhiwa pesa hizo ili alipe wafanyakazi mishahara, mdada huyo akatokomea kusikojulikana.
`Baadaye kidogo akaniambia kuwa anatoka kidogo baada ya kutumwa na Mkurugenzi huku akidai kuwa pesa ameziacha ofisini na atarudi baadaye kwa ajili ya kugawa mishahara… lakini tangu hapo hajaonekana,` akasema Bw. Masaoe.
Akasema kuwa awali, baada ya kuona akichelewa kurudi, akawasiliana naye kwa njia ya simu, lakini baadaye akazima simu kabisa.
Akasema baada ya hapo wakaamua kutoa ripoti polisi.
Akasema tayari amesharipoti kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Wazo Hill na kupata hati ya kumkamata, yenye namba WH/RB/4193/07.
Meneja huyo amesema baada ya tukio hilo, ilibidi zitafutwe pesa nyingine haraka na kuwalipa mishahara nusu wafanyakazi wa hoteli hiyo.
Bw Masaoe, ameongeza kuwa mbali na jina la Norin, pia wamegundua kuwa mtunza fedha wao huyo ana majina mengine kibao anayotumia.
Akayataja majina hayo kuwa ni Maria Mashauri, Furahini na Happiness.
Akaomba mtu yoyote atakayemuona mdada huyo apige simu namba 0755- 832768 au 0754 629009.
|