|
Yatima Mbweni wapewa misaada
2007-06-16 18:28:50
Na Moses Ismail, Mbweni
Asasi isiyo ya kiserikali ya Tuishi Salama Mbweni, juzi ilitoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu wa shule mbili za Kata ya Mbweni Jijini Dar es Salaam.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya jumla ya sh. milioni tatu, vimegawiwa kwa wanafunzi 150 wa shule za msingi za Mbweni na Kiungageni zote za Mtaa wa kiserikali wa Maputo.
Akizungumza na Alasiri wakati wa afla ya kugawa vifaa hivyo, ambavyo ni sare za shule, viatu, mabegi ya kuhifadhia madaftari na madaftari yenyewe, Mwenyekiti wa asasi hiyo, Bi. ClaraUrassa alisema msaada huo ni moja ya majukumu ya taasisi yake ambayo ilianzishwa kwa lengo la kusaidia watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu na pia kutoa misaada na ushauri kwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, VVU.
`Kama unavyoona, watoto wote hawa wanaishi katika mazingira magumu, na hili ni jukumu la jamii yetu kuwasaidia kwa hali na mali,` akasema Bi. Urassa.
Alisema msaada huo walioutoa umechangiwa na taasisi ya kimataifa ya RFA baada ya asasi yake kuiandika mchanganuo wa kuomba msaada kwa watoto wa Mbweni ambao wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na uyatima au kulelewa na mzazi mmoja.
Akasema mchanganuo waliouandika na kuwawezesha kupata msaada huo waliupitishia TACAIDS, ambao nao waliupeleka kwa RFA na kufanikisha kupata vifaa walivyotoa msaada kwa wanafunzi hao 150.
Akizungumza baada ya kupokea msaada wa watoto wake, Bi. Halima Ali, mama anayelea watoto wawili peke yake baada ya kufiwa na mumewe, alisema msada huo umempa nguvu ya kuendelea kuwalea watoto wake kwa upendo akiamini jamii bado iko na yeye.
Naye Katibu wa Tuishi Salama Mbweni, Bi. Fatuma Nasir, alisema kata ya Mbweni ni moja ya kata zenye tatizo kubwa la watoto waoishi katika mazingira magumu na wanahitaji misaada ya mara kwa mara.
|