|
Ajali mbaya ya Singida: Maharusi wateketea
2007-06-16 18:32:27
Na Mwandishi Wetu, PST - Singida
Wakati taifa bado limegubikwa na msiba mzito uliotokea jana kufuatia basi la abiria kupinduka na kisha kulipuka na kutetekea kabisa, imebainika kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha ni wapenzi wawili waliokuwa wakielekea kwao Mwanza kufunga ndoa.
Habari zilizopatikana kutoka kwenye tukio zinasema wawili hao walikuwa wanakwenda kukamilisha shughuli hiyo kwa wazazi baada mambo yote kuandaliwa Jijini Dar.
`Wapenzi hao walikuwa wakilia huku wakiagana…sauti zilisikika sana lakini baadaye zikafifia na kuisha kabisa,` mmoja wa watu wanaodai kufika eneo la tukio wakati basi hilo likiungua ameliambia gazeti hili kwa njia ya simu.
Ajali hiyo mbaya iliyohusisha basi la kampuni ya Mohammed Trans, aina ya Scania, lenye namba za usajili T 423 AFW, ilitokea jana saa kumi jioni kwenye kona kali iliyopo eneo la Kindai, umbali wa kilomita tano kutoka mjini Singida.
Basi hilo lilikuwa likitokea Jijini Dar kwenda Mwanza.
Kwa mujibu wa walioshuhudia, mara baada ya basi hilo kupinduka, lililipuka na kuwaka moto.
`Basi lilianza kuungua tangu saa kumi jioni lakini hadi saa moja usiku, moto ulikuwa bado unawaka sehemu ambazo tunaamini ndipo kulikuwa na miili ya watu,` mtu mwingine aliyekuwepo kwenye tukio amesema.
Kwa mujibu wa watu hao, abiria waliokuwa ndani ya basi hilo walipiga kelele wee kuomba msaada lakini ikashindikana kutokana na moshi kujaa ndani ya basi na pia kutokuwepo kwa gari la zimamoto.
`Idadi ya waliokufa ingekuwa ndogo kama kungekuwa na jitihada za kuokoa watu,` mmoja wa mashuhuda akaongeza.
Imeelezwa kuwa ilipofika saa moja, milipuko ambayo watu waliamini ni vichwa vya watu vinapasuka, ilianza kusikika nje ya gari hilo.
`Ukifika kwenye tukio utaangua kilio. Hakuna kilichobaki. Mali na miili ya abiria vyote vimeteketea na kubaki jivu…mwili pekee ulioonekana ni wa mtu mmoja ambaye inasemekana alikuwa konda wa basi hilo,` mmoja wa walionusurika katika ajali hiyo ameliambia gazeti hili kwa njia ya simu.
Amesema mara baada ya basi hilo kuanguka, ilichukua kama dakika tatu tu, likalipuka na kuanza kuwaka moto.
`Mimi nilibomoa dirisha la nyuma na kujiokoa. Pia niliokoa abiria kadhaa kabla ya basi kujaa moshi na moto mkubwa kuzuzuia kuingia kuokoa wengine,` akasema shujaa huyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Lawrence Tarimo alisema jana usiku kuwa waliokufa walikadiriwa kuwa zaidi ya 20.
Naye Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Aubrey Mushi alisema hadi jana jioni alikuwa amepokea majeruhi 42.
Wakizungumza na mwandishi wa PST, baadhi ya abiria walionusurika katika ajali hiyo wanasema chanzo hasa ni kupasuka kwa tairi mojawapo la mbele.
Wakasema baada ya hapo, basi lao liliyumba sana na kumshinda dereva kabla ya kupinduka na kulipuka moto.
Hata hivyo, wanasema mashuhuda kuwa hapo kabla, dereva wa basi lao alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi.
Wakasema wanaamini dereva wao aliamua kulikimbiza basi kwa kasi zaidi kwa sababu alikuwa akishindana na gari jingine la kampuni hiyo ya Mohamed Trans.
Wakasema wakati wakiwa kwenye kona moja kali ya eneo hilo la Kindai ndipo tairi lilipopasuka ghafla na gari lao kupinduka kabla ya kushika moto.
Wakasema mashuhuda hao kuwa mbaya zaidi, basi hilo lililalia upande ulio na mlango wa kawaida wa kuingilia na kutokea ndani ya basi, hivyo lilipoanza kuwaka moto, hali ilikuwa ngumu kwa abiria wote kuweza kujichomoa garini humo.
Wakasema abiria kadhaa walijaribu kujiokoa, lakini wakaishia kunasa kwenye madirisha na mwishowe kuangamia kwa moto mkali ulioliteketeza basi hilo.
|