|
Zamu ya Stars Ghana-Maximo
2007-06-18 18:53:44
By George John, Jijini
Wakati mashujaa wa Tanzania, Taifa Stars `JK Boys`, wakitarajiwa kuwasili Jijini Dar mchana huu wakitokea Dodoma baada ya kuwasili jana usiku Jijini Mwanza wakitokea Burkina Faso, kocha mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo amesema ni zamu ya Stars kucheza fainali za mataifa ya Afrika.
Maximo amesema hayo muda mfupi baada ya timu hiyo kuwasili Jijini Mwanza wakitokea Burkina faso ambako walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya taifa hilo la Afrika Magharibi.
Amesema kama ilivyo katika nyanja nyingine za maisha, kila jambo lina wakati wake na safari hii ni zamu ya JK Boys kushiriki fainali hizo.
Kwa ushindi huo, Stars imefikisha pointi 8 na kushika nafasi ya pili huku Senegal wakiendelea kuongoza kundi hilo la 7 wakiwa na pointi 8 kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.
Hata hivyo, Maximo amemrushia lawama mwamuzi wa mchezo huo kwa `kuikandamiza` Stars lakini akadai anamsamehe kutokana na ushindi ulioupata timu yake huku akitazama zaidi mbele.
Aidha, Mbrazil huyo amewashukuru Watanzania kwa mshikamano waliouonyesha kwa timu yao jambo ambalo hakulitarajia tangu alipoanza kuifundisha timu hiyo.
``Ushindi huu ni wa Watanzania wote na naamini tutamalizia kwa ushindi dhidi ya Msumbiji nyumbani,`` amesema.
Timu hiyo mara baada ya kuwasili Jijini Mwanza ililakiwa na viongozi mbalimbali wa serikali wa mkoa huo, viongozi wa soka pamoja na mashabiki waliokuwa wamejazana uwanja wa ndege licha ya kuwa na giza `nene`.
Kwa upande wake, mfungaji tegemeo wa Stars, Nizar Khalfan amesema mchezo huo ulimkataa lakini kama zilivyo timu nyingine, mchezaji yeyote ana nafasi ya kufunga.
``Ni kawaida siku nyingine `gemu` kukataa, lakini kila mmoja ana nafasi ya kufunga katika timu hovyo nimefarijika na ushindi,`` amesema.
|