|
TAKUKURU yaeleza ilivyomnasa Mhadhiri anayedaiwa kupokea mlungula
2007-08-21 16:39:31
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa nchini, TAKUKURU imeeleza namna ilivyoweza kumnasa mkufunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam anayedaiwa kupokea rushwa ya Dola 1,000 za Kimarekani ili amruhusu denti wake mmoja kufanya mtihani aliokuwa ameukosa.
Taarifa ya taasisi hiyo imemtaja mkufunzi aliyedakwa katika mtego wao kuwa ni Nehemi Stephen Kekeza wa Kitivo cha Sheria chuoni hapo.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Elimu kwa Umma ya TAKUKURU imedai kuwa mkufunzi huyo aliomba rushwa ya dola za Kimarekani 1000 kutoka kwa mwanafunzi wake ambaye alishindwa kufanya mtihani kwake kwa sababu alizodai kuwa hazikuweza kuzuilika.
Ikasema taarifa hiyo kuwa mwanafunzi huyo baada ya kushindwa kufanya mtihani huo kwa wakati, baada ya kumaliza matatizo yake, ndipo akamfuata mwalimu wake na kumuomba ampe mtihani huo aufanye ili apate sifa za kuendelea na masomo kwa mujibu wa taratibu za chuo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkufunzi huyo alikataa kumpa mtihani huo kwa sharti kwamba mpaka alipwe dola 1,000 za Kimarekani, ikiwa ni namna mojawapo ya kumsaidia ili afanye mtihani huo.
Inasema taarifa hiyo kuwa mwanafunzi huyo aliamua kutoa taarifa hiyo TAKUKURU, ambayo iliandaa mtego uliofanikisha kumdaka mwalimu huyo kiulaini kabisa.
`TAKUKURU iliandaa mtego wa fedha hizo kama alivyokuwa ameomba mkufunzi huyo na mtego ulifanikiwa kwa Mkufunzi Kekeza kupokea pesa hizo katika ofisi yake nyingine iliyoko Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam na kukamatwa na maofisa wa TAKUKURU,` ikasema Taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mkufunzi Kekeza angepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam.
|