|
Vigogo wa CCM Dar waombwa kuwatimua wanaomwaga pesa wawe viongozi
2007-08-23 18:31:54
Na Abdul Mitumba, Jijini
Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Dar es Salaam, imeombwa kuwa makini na maamuzi yake ili isijikute ikitoa maamuzi yasiyozingatia maslahi ya chama wakati wakiushughulikia tuhuma mbalimbali dhidi ya wanachama wanaojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kusaka viongozi.
Ombi hilo limetolewa na wana CCM wa kata za Mzimuni, Mwananyamala na Makumbusho, kufuatia kamati hiyo kuweka kando suala la kuwepo kwa uhasama miongoni mwa wanachama katika kata ya Makumbusho.
Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 15 akiwemo Mkuu wa mkoa na Mstahiki Meya wa Jijini la Dar es Salaam, imekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuahidi kulishughulikia baada ya chaguzi ngazi zote kumalizika.
Kwa mujibu wa barua ya kamati hiyo ya Agosti 16 kwenda ofisi za CCM wilaya ya Kinondoni, imeagiza matawi yote ambayo chaguzi zake zilikwama zifanyike zikishirikisha wanachama wote.
Barua hiyo ilifafanua kuwa inatambua ukubwa wa tatizo lililoyakumba matawi sita kati ya tisa ya kata ya Makumbusho na kusababisha chaguzi zake kukwama.
Akizungumza na Alasiri, Mwenyekiti wa CCM kata ya Mzimuni, Bw. Hassan Mwambe amesema mizengwe katika chaguzi inaweza kukiangusha chama siku zijazo.
Naye katibu wa CCM kata ya Mwananyamala, Bw.Ally Mwingira, amesema kuwepo kwa malalamiko katika chaguzi ngazi za chini kunaweza kupandikiza chuki chaguzi ngazi za juu.
Kauli za viongozi hao zinatokana na Kata ya Makumbusho kukumbwa na kashfa za baadhi ya wanachama wake kukamatwa usiku wakiwa katika ukumbi mmoja eneo la Boko na kusababisha uchaguzi kusimamishwa hadi uliporudiwa juzi na jana.
Matawi yaliyokumbwa na mzozo huo ni Minazini, Ubuyuni, Makumbusho, Mchangani, Sindano na Kisiwani.
|