|
Shule `mbavu za mbwa` kujengwa upya kwa Sh. Mil 49
2007-08-23 18:32:56
Na Mary Wejja, Kunduchi
Hatimaye Shule ya Msingi Salasala iliyokuwa ikionekana kuwa ya kichovu zaidi katika Kata ya Kunduchi kutokana na majengo yake ya tope na paa la nyasi, sasa itakuwa ni miongoni mwa shule kali zaidi baada ya kuamuliwa kuwa itajengwa upya kwa gharama zinazozidi Sh. Milioni 49.
Akizungumza na Alasiri jana, Diwani wa kata hiyo, Bw. Patrick Makoyola, amesema shule hiyo ya udongo na nyasi, na ambayo ilijengwa kwa nguvu za wananchi wa eneo hilo, sasa itakuwa ni moja kati ya shule za kuvutia.
Akasema ujenzi huo mpya umeshaanza na kwa mara nyingine, ni wananchi ndio wanaojenga kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni pamoja na baadhi ya wahisani, ikiwemo Shule ya Kimataifa ya Even Of Piece ambayo imeahidi kusaidia uchimbaji wa kisima cha maji safi.
Akasema madarasa yanayojengwa yatachukua wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la nne na kubainisha kuwa wataendelea na ujenzi wa vyumba viwili viwili kila mwaka ili waweze kufikia hatua ya kuchukua wanafunzi hadi darasa la saba.
Bw. Makoyola akasema kuwa katika jitihada za kupanua wigo wa elimu zaidi, wananchi wa eneo hilo wameshatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari itakayoanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Akasema kuwa ujenzi wa shule ya Sekondari utaanza mara baada ya ujenzi wa Shule ya Msingi kukamilika kwa jitihada za nguvu za wananchi, wahisani pamoja na Manispaa ya Kinondoni.
Aidha, amesema kuwa wananchi hao pia wametoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, kufuatia kero inayowakabili ya kutokuwa na kituo cha afya katika kata nzima ya kunduchi hivyo kutoka huduma ya kulaza wagonjwa.
Katika hatua nyingine ya kuongeza jitihada katika kupanua wigo wa elimu katika kata hiyo wananchi wa eneo la Tegeta hivi karibuni walikaa kikao ambacho kilijadili utoaji wa eneo la Shule ya Msingi Pwani iliyopo Tegeta ili lijengwe Shule ya Sekondari itakayohudumia wakazi wa Tegeta Ununio, Kondo pamoja na Boko.
|