23 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mkakati waja kuwadaka wateja watakaokutwa wakinunua bidhaa za Machinga barabarani
 
2007-08-23 18:34:00
Na Francisca Jeremiah, Kinondoni

Ili kutokomeza tatizo la Machinga, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekuja na mkakati kabambe wa kuhakikisha inawakamata watu wote watakaokutwa wakinunua bidhaa toka kwa wafanya biashara hao barabarani na kuwaburuza kortini.

Aidha utaratibu huo utawahusu pia wale wote ambao watakutwa wakiuza bidhaa hizo maeneo ya makutano na katika taa za barabarani kama Morocco, Ubungo na Magomeni ambapo biashara hizo zimeshamiri.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Fabiani Massawe ofisini kwake, Jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akifanya mahojiano na gazeti hili.

Amesema Serikali inawataka Wamachinga wote kuuza bidhaa zao katika masoko waliyopangiwa ambapo wanunuzi wote watatakiwa kufuata mahitaji yao huko na si kununua ovyo barabarani.

`Lengo la kuanzisha kampeni hiyo ni kuhamasisha jamii ijenge utamaduni wa kufuata mahitaji yao sehemu husika na si kununua ovyo mitaani, naamini jamii ikiweza kufanikisha zoezi hilo, basi Machinga wa barabarani wataweza kutulia katika masoko waliyopangiwa,` akasema Kanali Massawe.

Amesema utaratibu huo unatarajiwa kuanza mwezi mmoja ujao.

Amewataka viongozi wa ngazi zote katika wilaya yake kuonyesha ushirikiano wa utendaji wa kazi za kijamii na kiofisi , kwa kutatua matatizo yaliyopo ili waweze kujiletea maendeleo.

`Kila kiongozi akitekeleza wajibu wake pasipo kusukumwa, basi tutafanikiwa zaidi kudhibiti uharifu na kuondoa matatizo yaliyopo, kwani wilaya hii husifika kwa uovu mwingi, sasa tunataka kuibadilisha kwa kuanzisha mikakati mbalimbali ya kupambana nayo,` akaongeza.

Aidha amewataka wana jamii kuacha mazoea ya kuyakumbatia maovu kwa kuwatetea wahalifu, bali wawe mstari wa mbele kuyafichua kwa kutoa taarifa katika ofisi yake na kwenye vituo vya polisi au hata kwa watendaji wa mitaa ili weweze kushughulikiwa.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.