|
Shule za sekondari 20 kunufaika na Mradi wa Stadi za Maisha
2007-08-23 18:34:58
Na Grace Chilongola, PST
Jumla ya sekondari 20 za Manispaa ya za Temeke na Kinondoni zitanufaika na Mradi wa Stadi za Maisha utakaoendeshwa na asasi moja isiyo ya Kiserikali iitwayo FRAT, imeelezwa.
Katika mahojiano na PST wakati wa utambulisho wa Mradi wa Stadi za Maisha katika Manispaa ya Temeke, Mkurugenzi wa asasi hiyo, Bi. Juliana Bwire, amesema wafadhili wao Family Health International (FHI) wamewapatia zaidi ya Sh. Mil. 100 kwa ajili ya kupanua mradi huo.
Akasema katika awamu hii, mradi huo utashughulika na shule 20, ambapo 10 zitakuwa za manispaa ya Temeke na 10 manispaa ya Kinondoni.
Akasema mafanikio yaliyoonekana katika mradi huo wakati ukiwa kwenye manispaa ya Kinondoni ndio yaliyowafanya wafadhili wao kuwaongeza pesa kwa ajili ya kusambaza huduma hiyo katika Manispaa ya Temeke.
Aidha, akazitaja shule zitakazonufaika kuwa ni pamoja na sekondari za Chang`ombe, Kibasila, Temeke, Jitegemee, Maarifa, Nurulyakini, Tandika, Makangarawe, Kigamboni na Kurasinim zote za Manispaa ya Temeke.
Kwa Kinondoni, shule zitakazonufaika na mradi huo ni sekondari za Magomeni , Kambangwa, Perfect Vision, Mbezi Beach, Biafra, Kijitonyama, Tegeta, Cambrige, New Horizon na Mama Salma Kikwete.
Naye Afisa elimu Taaluma mkoa wa Dar es Salaa Bw. Silas Samaluku akawataka vijana kuwa na maamuzi yaliyo sahihi katika suala la ukimwi.
|