|
Kata ya Ndugumbi yawapiga marufuku wazoa taka...
2007-08-23 18:37:13
Na Sabato Kasika, Jijini
Wazoa takataka wanaotumia mikokoteni kufanya kazi hiyo, wamepigwa marufuku kwenye kata ya Ndugumbi Jijini, kwa madai kwamba wanachangia kuchafua mazingira ya kata hiyo.
Agizo hilo limetolewa na diwani wa kata hiyo, Bw. Charles Mgonja wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kisiwani, akiwa katika ratiba yake ya mikutano ya hadhara, anayoifanya ili kujua kero za wananchi wake.
Diwani huyo amedai kuwa amefuatilia kwa makini mambo mbalimbali kwenye kata hiyo na kubaini kwamba, watu wanaopita mitaani na kukusanya takataka wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kuchafua mazingira ya maeneo Jijini, likiwemo hilo la kata yake.
`Hawa watu hawana sehemu yoyote ya kupeleka takataka na badala yake wanakwenda kuzimwaga kwenye barabara ya Morogoro...kuanzia sasa sitaki kusikia kwamba wanapita mitaani na kukusanya taka, tumieni wakandarasi wanaokuja na malori,` akasema Bw. Mgonja.
Amefafanua kuwa kila kata ina wakandarasi wa kuzoa takataka ambao hupita wakizikusanya kwa magari yao na kuzipeleka kunakohusika.
Akasema wakandarasi hao hawafanyi kazi kama wale wanaotumia mikokoteni ambao huchukua pesa na kwenda kumwaga takataka hizo katika barabara ya Morogoro, jambo linaloongeza uchafuzi wa mazingira ya barabara hiyo.
`Kwanza kabisa nyie wenyewe muwakatae na wala msiwape pesa kwa ajili kuwazolea takataka zenu, fuateni utaratibu kwa kuwatumia wakandarasi ambao wamewekwa rasmi kwa kazi hiyo na wala msitafute unafuu ambao unachangia kuchafua mazingira yenu,` akasema diwani huyo.
Aidha, katika mkutano huo, wakazi wa mtaa huo walidai kuwa ukosefu wa maji ya bomba ni moja ya kero kubwa zinazowakabili kwa muda mrefu ambapo walimuomba diwani huyo kushughulikia kero hiyo haraka ili wasiendelee kuteseka kwa kunuanua ndoo moja ya maji kwa Shilingi 700.
Mbali na kero hiyo, wakazi hao wamedai kwamba, wamekuwa wakitozwa fedha katika kituo kidogo cha Polisi kilichopo eneo hilo, kwa ajili ya dhamana wanapokwenda kuwatoa ndugu zao wanaokamatwa kwa makosa mbalimbali.
Wananchi hao wakamuuliza diwani wao ikiwa ni halali kutoa pesa kituo cha polisi, wakati wa kumdhamini mtu.
Diwani huyo anatarajia kuendelea na mikutano yake kwenye mitaa mingine Ijumaa wiki hii ambapo atakuwa kwenye mitaa ya Kagera Mikoroshini.
|