24 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Walioathirika na VVU waombwa kutangaza vipimo vyao
 
2007-08-24 18:25:18
Na Mary Wejja, Mwananyamala

Wananchi waliojitokeza kupima ukimwi kwa hiari hivi karibuni kwa nia ya kuunga mkono kampeni iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete wamepongezwa kwa hatua hiyo na sasa kutakiwa kukubali changamoto nyingine ya kutangaza matokeo ya vipimo vyao ili ijulikane kama wameathirika ama la.

Akizungumza na Alasiri ofisini kwake Jijini, Mratibu wa Mtandao wa Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini, TANOPHA, Bw. Bruno Ghumpi, amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza kasi ya maambukizi.

Akasema, itamsaidia pia mhusika kuepukana na vishawishi vitakavyomsababishia kuongeza tatizo zaidi na kuzalisha maambukizi mapya.

Aidha amesema kuwa, ingawa hatua ya upimaji wa virusi vya ukimwi kupitia kampeni inayoendelea ni nzuri, lakini kasoro inayojitokeza ni katika suala la ufinyu wa muda wa utolewaji wa ushauri nasaha.

``Mtu anapofikia maamuzi ya kupima anatakiwa apate ushauri nasaha wa kutosha kabla ya kupima, lakini kwa kuwa kunakuwa na kundi kubwa la watu wanaojitokeza kupima kwa wakati mmoja, unakuta watu hawa hawapati nafasi ya kutosha katika kupata ushauri nasaha, `` akasema Bw.Ghumpi.

Akaongeza kuwa tatizo hilo la ukosefu wa muda wa kutosha wa utolewaji wa ushauri nasaha, linaweza kusababisha madhara kwa mtu ambaye vipimo vyake vimeonyesha kuwa hajaathirika kwa sababu anaweza kujiona mshindi na kufanya mambo ambayo yatamuingiza katika hatari ya kupata maambukizi.

Hata hivyo, Bw.Ghumpi ameiomba serikali kuweka wazi suala la namna ya kuwasaidia watu ambao watabainika kuwa wanaishi na virusi vya ukimwi na pia kubainisha aina ya msaada watakaowapatia mara baada ya kugundulika kuwa wameathirika na ugonjwa huo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.