24 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Madereva teksi Jijini waicharukia
 
2007-08-24 18:28:55
Na Job Ndomba, Mikocheni

Baadhi ya madereva teksi Jijini wamekijia juu chama cha Madereva Teksi nchini cha Tunawajali wakikitaka kisiingilie majukumu ya Serikali kwa kuwa si msemaji wao.

Wamesema chama hicho hakitambuliki kwa madereva wote kwa vile ni cha hiari na hivyo kinawahusu wanachama pekee.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya chama hicho kutaka Serikali isajili haraka vituo vya teksi.

Madereva hao wamelalamika wakati wakizungumza na Alasiri katika ofisi zake zilizopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

Wamesema chama hicho ni cha hiari na hivyo si busara kuwa msemaji wa madereva wote kwani hata Halmashauri zinafahamu hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw.Fuad Latiff wa kituo cha teksi cha Palm Beach, amesema msemaji wa chama hicho amekiuka taratibu, kwa kujifanya msemaji wa madereva wote nchini badala ya kuwajibika kwa wanachma wake pekee.

Bw. Latiff amesema awali msemaji wa chama hicho alitoa taarifa kwenye moja ya gazeti la kila siku, akisema kuwa madereva wametaka vituo visajiliwe haraka, kauli ambayo imepingwa vikali.

``Huyo jamaa aliyeongea, si msemaji wetu, bali anaweza kuzungumzia suala hilo kwa wanachama wake pekee na si kwa madereva wa nchi nzima, kwani sisi tunaweza kujiunga na chama chochote na si Tunawajali pekee,`` akasema Bw. Latiff.

``Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala inawahakikishia kuwa chama hicho ni cha hiari, hakina haki ya kisheria kuwalazimisha au kuwashawishi kuanzisha vituo vya teksi pasipo ridhaa ya mamlaka ya Manispaa ya Ilala,`` imesema sehemu ya barua iliyotolewa kwa madereva teksi hao.

Aidha barua hiyo imesema madereva hao wanayo haki ya kukataa maelezo yoyote kutoka kwa chama hicho kuhusu uanzishwaji wa vituo vya teksi.

Barua hiyo imesisitiza kuwa licha ya Manispaa ya Ilala kukitambua chama hicho, lakini haijatoa jukumu kwa chama hicho au chama chochote kusimamia uandikishaji vituo au upasishaji wa teksi.

Majukumu hayo yapo chini ya afisa wa Halmashauri za Manispaa kwa kuzingatia sheria na kanuni na taratibu zilizowekwa, imesema barua hiyo.

Naye Bw.Mohamed Rajabu wa kituo cha Mkunguni na Lumumba,amekitaka chama cha Tunawajali kuwa msemaji kwa wanachama wake tu na si kwa kila dereva wa teksi.

Aidha Bw. Rajabu ameiomba Serikali kupitia mamlaka yake kufanya uchunguzi wa kina katika chama hicho ili kupunguza migongano, kwani chama hicho si mwakilishi halali kwa madereva teksi wote nchini.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.