|
Mateja wengine 20 wabwaga manyanga
2007-08-24 18:30:27
Na Francisca Jeremiah, Ilala
Ziara iliyofanywa na Meya wa Manispaa ya Ilala Bwana Abuu Jumaa, kutembelea maskani zote za mateja, imeanza kuzaa matunda baada vijana hao kujisalimisha kwake na kuahidi kuacha kwa hiari yao utumiaji wa madawa ya kulevya.
Hayo yamesemwa na meya huyo wakati alipokutana na wadau kufanya tathimini ya ziara hiyo, katika ukumbi wa Manispaa.
Amesema vijana wapatao 20 wamejitokeza na kuahidi kuacha kabisa utumiaji wa madawa hayo baada ya kupatiwa ushauri kuhusiana na madhara ya kiafya yanayosababishwa na unga.
``Kuna umuhimu wa kuwajali vijana hao kwa kuwapatia misaada na ushauri ambao utawasaidia ili waweze kurudi katika hali yao ya awali,`` amesema Maya Jumaa.
Katika ziara yake hiyo aliongozana na wadau mbalimbali ambao walisaidiana kuwashauri vijana hao kuachana na kazi hiyo na wajihusishe na kazi za kuisaidia taifa.
Aidha meya huyo amesema kutokana na mafaniko waliyoyapata kwa kuwashawishi vijana hao kuacha utumiaji wa madawa , manispaa imeandaa mkakati wa kujenga kituo cha kuwahudumia vijana hao.
``Tunachotaka kufanya sasa ni kuitaka jamii iweze kusaidiana nasi kwa kujitolea michango ili tuweze kujenga kituo cha kuweza kuwasaidia vijana hao, ambacho kitakuwa kikiwahudumia kwa kuwapatia ushauri na misaada mingine,`` akasema Maya Jumaa.
Mbali na hayo amesema vijana hao watasaidiwa kwa kupewa ajira za muda zitakazokuwa zinatolewa na manispaa hiyo.
Amesema ajira hizo zitatokana na miradi mbalimbali itakayobuniwa na jamii kama ile ya kusafisha mazingira, utunzaji wa bustani za maua na miti.
Zingine ni ujenzi wa barabara na usimamiaji wa shughuli mbalimbali zitakazoendeshwa na manispaa hiyo.
Meya Jumaa ameitaka jamii nzima hususani wazazi kutoa ushirikiano katika kudhibiti utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana wao.
|