|
Moto waleta kilio kingine Jijini Dar
2007-08-24 18:31:46
Na Kiyao Hoza, Polisi Kati
Siku chache tu baada ya moto kulipuka kwenye nyumba mbili tofauti Jijini na kuwasababishia umauti watu saba pale Kimara na Mbezi, ajali nyingine ya moto imetokea usiku wa kuamkia leo na kusababisha hasara kubwa kwa wahusika.
Taarifa inasema moto huo uliosababishwa na mshumaa uteketeza vyumba vinne na mali zote zilizokuwamo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Masindoki Masindoki, ameiambia Alasiri leo asubuhi moto huo umeteketeza mali nyumbani kwa Bi. FatumaMohamed, 85, mishale ya saa 6.40 usiku wa kuamkia leo.
Akasema tukio hilo limetokea katika makutano ya mitaa ya Lindi na Shauri Moyo na kuteketeza vyumba vinne vya wapangaji kati ya vyumba 10 vya nyumba hiyo.
Amewataja wapangaji waliothirika na ajali hiyo kuwa ni wale waliopanga kwenye mabanda ya nyumba hiyo ambao ni Bw. Mohamed saidi, 54, Bakari Issa, 33, Kirusia Ayubu, 28 na Saidi almarufu kama Mpemba.
Kamanda Masindoki amesema thamani halisi ya mali zilizoungua bado haijafahamika na hakuna madhara kwa binadamu.
Aidha, amesema chanzo cha moto huo ni mshumaa uliowashwa chumbani kwa Mpemba na kuachwa ukiwaka hadi uliposababisha ajali hiyo.
Ameongeza kuwa moto huo ulifanikiwa kuzimwa na kikosi cha Zimamoto cha Jiji.
|