|
Ajari ya gari yajeruhi watu wanne
2007-08-24 18:33:07
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili
Watu wanne akiwemo utingo wa gari, wamejeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya fuso walilopanda kuporomoka bondeni likiwa na shehena kubwa ya magunia ya unga.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa tano asubuhi katika kijiji cha Sotele wilaya ya Mkuranga, ambapo gari hilo aina ya Fuso lenye namba ya usajili T 575 ACD lilipinduka baada ya kufeli breki wakati likishuka mlima.
Hata hivyo kwa watu wanaoishi eneo la tukio, ajali hiyo ilikuwa kama neema kwao kwani walijipendelea kwa kubeba magunia vichwani na kuingia nayo mitini.
Watu waliojeruhiwa katika tukio hilo wametambuliwa kuwa utingo wa lori hilo Hamisi Hassan, 38, na wafanyabiashara Selemani Mohamed, 25, Waziri Ahmed Makundi na Mzee Mikidadi, ambao kwa sasa wamelazwa katika wodi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa, MOI, wakipatiwa matibabu.
Akisimulia tukio zima, Hamisi amesema lori hilo lilikuwa limebeba maguni 130 ya unga yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda eneo la Kisiju kwa ajili ya kusambazwa madukani.
Akasema walipofika eneo la tukio, gari lao lilianza kushuka mlimani, lakini walipofika katikati ya mtelemko, ghafla gari likaanza kuchanganya mwendo na hapo ndipo walipotambua hali ya hatari iko mbele yao kufuatia breki ya gari hilo kukatika.
``Dereva alitoa onyo kuwa gari limemshinda kwani breki zimekatika…kila mtu alianza kuomba kwa mungu anayemjua ili amuokoe na hatari ile,`` akasema Bw. Hamisi.
Kwa mwendo wa kasi, gari hilo liliacha njia na moja kwa moja likaelekea bondeni na kupinduka mara kadhaa na kusababisha magunia ya unga kuwafunika na kuwakandamiza.
Ameongeza kwamba, baada ya gari kupinduka, wao walikuwa katika hali mbaya, kitu ambacho kilisababisha watu waliowahi kwenye tukio kuchukua baadhi ya magunia na kwenda nayo misituni.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa amesema watu hao walifikishwa hapo jana majira ya saa moja usiku, ambapo kwa haraka waliwahishwa katika chumba cha upasuaji wa dharura na kupatiwa huduma.
|