24 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Vurugu zafumka wodini Muhimbili
 
2007-08-24 18:35:51
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, vurugu kubwa zimefumka katika wodi moja ya Hospitali ya Taifa Muhimbili hivi karibuni baada ya mgonjwa mmoja kubaini kuwa mgonjwa aliyelazwa naye jirani ni jambazi hatari na ndiye aliyeshiriki kumcharanga mapanga usiku hadi akafikishwa wodini hapo.

Tukio hilo lililozua kitimtim cha aina yake na kuwaacha manesi na madaktari midomo wazi, liliwalazimu askari polisi kadhaa kuitwa na hatimaye kumchomoa wodini mgonjwa anayetuhumiwa kuwa jambazi.

Sakata lenyewe lililoanza kama mchezo wa kuigiza kabla ya kuzua tafrani linasimuliwa na mashuhuda kama ifuatavyo:
Kwamba alfajiri ya Agosti 21, mtu aitwaye Kamili John, 50, mkazi wa Msasani Jijini alifikishwa katika wodi 17 ya Jengo la Sewahaji akiwa hoi baada ya kuvamiwa na majambazi, kuporwa mapesa na kisha kucharangwa mapanga katika sehemu kadhaa za mwili wake.

John akapata matibabu ya awali na kupewa dawa ambazo zilimfanya apatwe na usingizi mzito.

Mara, wakati akiwa usingizini, wodini humo akaletwa mgonjwa mwingine (jina tunalo).

Inaelezwa kuwa huyu alifikishwa hapo akiwa amejeruhiwa vibaya mkononi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni matokeo ya kipigo toka kwa watu wasiofahamika.

Huku wodini kukiwa shwari, mara mgonjwa John akaamka toka kwenye usingizi mzito.

Ile anapepesa macho, akashangaa kumuona mgonjwa huyo aliyelazwa jirani yake.

Ghafla akaanza kugumia, akisema kuwa mgonjwa mwenzie huyo ni mmoja kati ya majambazi waliomvamia usiku wa siku hiyo na kumcharanga mapanga hadi kumfanya awe hoi hospitalini.

Inaelezwa kuwa yule mgonjwa mwingine akabaki kutumbua macho kabla ya kujitetea kuwa siye.

\"Hapo ndipo vurugu zilipofumka,\" amesema mmoja wa wahudumu wa wodi hiyo.

Inaelezwa kuwa John akazidi kupiga kelele akitaka jamaa huyo aliyemwita jambazi akamatwe.

Baada ya hapo wagonjwa wengine wakaungana naye baada ya kudai kuwa kisa cha mgonjwa huyo kufikishwa hapo ni pigo moja la panga ambalo majambazi wenzie walikosea katika mapambano kwa kumkata wakati wakimshambulia yeye.

Yule mgonjwa mwingine akajitetea kuwa yeye aliumia wakati akicheza disko katika ukumbi mmjoja Jijini.

Baada ya vurugu kuzidi na kelele kusikika huku na huko, ikaelezwa kuwa askari polisi wakaarifiwa ambapo kwa haraka, kundi kubwa likatinga wodini na kufanya taratibu za kumchomoa wodini huku akiwa chini ya ulinzi mkali.

``Polisi walipowahoji wagonjwa wote wawili, yule anayetuhumiwa kwa ujambazi akawa hana maelezo ya kutosha kuhusiana na majeraha yake na ndipo walipombeba na kuondoka naye,`` akasema muuguzi mmoja.

Alipoulizwa kuhusu sakata hilo, Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI, Bw. Almas Jumaa, akakiri kwamba hali haikuwa shwari na ndio maana polisi wakaitwa.

Hatahivyo, akasema walimruhusu mgonjwa mwingine kutolewa wodini na polisi kwa sababu hali yake ilikuwa njema baada ya kutibiwa.
Mgonjwa John bado amelazwa wodini hapo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.