25 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waislamu Dar kuujadili Mfungo wa Ramadhani
 
2007-08-25 19:17:14
Na Badru Kimwaga, Jijini

Waumini wa dini ya Kiislam Jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani wanatarajia kukutana pamoja kuanzia leo kwenye kongamano la siku mbili litakalojadili mapokezi ya mwezi wa mfungo wa Ramadhani na mambo mengine kadhaa ya kimaendeleo.

Kongamano hilo litafanyika katika viwanja vya Bakhresa pale Manzese Jjini.

Taarifa zinasema kongamano hilo litakaloongozwa na wahadhiri na masheikh mbalimbali maarufu nchini, limeandaliwa na Baraza la Habari la Kiislam Tanzania, BAHAKITA na litaisha kesho Jumapili.

Mkurugenzi wa BAHAKITA, Ustaadh Hussein Msopa, ameliambia Alasiri kuwa kongamano hilo litakuwa na ajenda kuu mbili ambazo ni kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Waislam katika Mapambano ya Ugonjwa wa Ukimwi.

Msopa amesema masheikh kadhaa maarufu watashiriki katika kuwasilisha mada hizo kwa waumini watakaohudhuria akiwemo Dk. Sulley, Jumanne Amir yeye mwenywe na wengineo kadhaa walioalikwa.

Mkurugenzi huyo amesema katika mada ya Uislam na Ukimwi, watazungumzia umuhimu wa waumini wa dini hiyo nayo kushiriki katika mapambano ya Ukimwi kwa kushirikisha viongozi wao ikiwemo kujitokeza kupima na kujitangaza hadharani.

``Unajua Rais Jakaya Kikwete ameshaonyesha njia na kutoa wito kwa wananchi wote kushiriki vita hivi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama dhiid ya virusi, nasi kama taasisi ya kidini tumeitikia wito kwa kuliitisha kondamano hilo,`` Chiepf Msopa amesema.

Ameongeza kuwa mbali na mada hizo kuu mbili, pia wahadhiri na masheikh hao watashiriki kwa pamoja kujadili mikakati na maendeleo ya Waislam wa Tanzania katika nyanja mbalimbali za kielimu, kiuchumi, kiutamaduni na hata kisiasa.

Akasema kibali kwa ajili ya kongamano hilo linalotarajiwa kuanza saa 8:00 mchana kimeshapatikana na Mgeni Rsmi atakuwa Kamishna mmojawapo wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini, Ustaadh Othman Ntaru.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.