|
DC awacharukia `mungiki` wa Dar
2007-08-25 19:18:19
Na Abdul Mitumba, Kinondoni
Seriakali wilayani Kinondoni Jijini Dar es Salaam imetangaza vita dhidi ya vikundi vya watu wanaojihusisha na uporaji mali za watu na kujifananaisha wauaji wa kundi la Mungiki wanaotingisha katika nchi jirani ya Kenya.
Aidha, Serikili imesema imebaini maeneo ambayo hutumiwa na vikundi hivyo katika kujibanza na kuwadhuru raia wema, hivyo iko katioka operesheni kali ya kusambaratisha kundi hilo na sasa askari kanzu wameshamwagwa katika kona husika ili kuwanasa.
Aliyetoa maelezo kuhusiana na wahalifu hao ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kanali Mstaafu Fabiana Massawe.
``Taarifa zilizoifikia ofisi yangu zinaonyesha vikundi hivyo vinapatikana katika maeneo ya manne tofauti yakiwemo Ubungo na Mwenge… lakini tumeshatoa tahadhari kwa wanaojihusisha na vikundi hivyo na pia operesheni ya kuwasaka imeshaanza,`` amesema Kanali Massawe.
Akaongeza kuwa kuwepo kwa vikundi hivyo ni batili na tena ni uvunjaji wa sheria za nchi.
Hatahivyo, Mkuu huyo wa wilaya amesema `Mungiki` wa Tanzania hawalingani na wa Kenya kwa sababau hutumia zana ndogo katika kutisha watu kabla ya kuwapora mali zao, ikiwa ni pamoja na visu, mapanga, bisibisi na ncha za chupa zilizovunjwa.
``Tunatambua kuwepo kwao na sisi kama Serikali tumejipanga vya kutosha katika kukabiliana nao,`` akasema Kanali Mstaafu huyo.
Kauli ya DC Massawe imekuja siku chache baada ya Mkutano wa wakuu wa wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke na watendaji wengine kufanyika hivi karibuni ambapo miongoni mwa yaliyojadiliwa ni kuwepo kwa Mungiki ambao hutishia usalama wa wakazi Jijini.
|