25 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Tapeli la mitihani latua Dar
 
2007-08-25 19:22:05
Na Job Ndomba, Jijini

Kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni matapeli hatari limeibuka Jijini Dar es Salaam na staili mpya ya wizi ambapo linawakomba wazazi mamilioni ya fedha kwa kuwalaghai kwamba litawafaulisha watoto wao mitihani ya kidato cha nne.

Ili wananchi wasiwe na wasiwasi nao, matapeli hao huongopa kwamba wanafanya kazi kwa ushirikiano na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa, (NECTA).

Dau la matapeli hao ni Sh. 150,000 kwa mwanafunzi anayetaka kufaulu kwa daraja la tatu, Sh. 200,000 daraja la pili na Sh. 300,000 kwa daraja la kwanza na mzazi hutakiwa kutoa pesa za awali na kisha kumalizia kiasi kilichobaki baada ya matokeo.

Hata hivyo, Alasiri ilipotaka kujua msimamo wa Baraza la Mitihani kuhusiana na suala hilo, ilielezwa wazi kwamba ofisi yao haihusiki kwa namna yoyote na ikashauri gazeti hili kuripoti suala hili polisi ili sheria ifuate mkondo wake.

Akizungumza na Alasiri, Naibu Katibu Mtendaji wa NECTA Bw. Thobias Oseno alisema haiwezekani kwa mtumishi wa baraza hilo aliyeteuliwa na rais kufanya mambo kama hayo.

Alisema watu hao ni matapeli na akawataka wananchi kutoruhusu mchezo huo na kwamba atakayebahatika kuwanasa, basi atoe taarifa kwa vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

``Hao watu wameamua tu kutumia jina la Katibu Mtendaji ili waweze kuhalalisha dili lao kwa nia ya kujipatia fedha,`` akasisitiza.

Hata hivyo, tayari kinara wa dili hilo ameshadakwa na anaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi Makao Makuu.

Mtuhumiwa huyo alidakwa na makechero wa Polisi maeneo ya Ubungo River Side wakati akifanya mazungumzo na mteja wake mmoja.

Polisi wanasema mtuhumiwa huyo aliyejitambulisha kwa jina la Yohana Charles na mwalimu wa masomo ya ziada `Tuition` kule maeneo ya Sinza, baada ya kupekuliwa, alikutwa akiwa na kitambulisho kinachomtambulisha kuwa yeye ni John Charles, mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Hihglands ya mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka Makao Makuu ya Polisi, baada ya nyumba ya mtuhumiwa kupekuliwa, pia zilikutwa nyaraka zenye majina lukuki ya wanafunzi na shule wanakotokea na alama za kila somo ambalo mwanafunzi anataka afaulishwe na daraja analotaka kupata.

Polisi wameliambia gazeti hili kwamba wanaendelea kumhoji mtuhumiwa ili kujua watu wengine wanaoshirikiana naye kwenye mradi huo haramu.

Awali mtuhumiwa huyo akiwa na kundi lake walidai kuwa wanashirikiana na ofisi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa na kwamba wana uwezo wa kuwatengenezea wanafunzi hao alama bora (Credit) kwenye mitihani yao.

Kundi hili lilikumbana na mwandishi wa habari hizi wakati likihaha katika shule mbalimbali Jijini na kumshawishi wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani.

Baada ya kuwashawishi wanafunzi na kukubaliana na wazo hilo, hatua ya pili ilikuwa ni kuongea na wazazi na kuwatajia viwango vya malipo kwa kila daraja ambalo wanataka watoto wao wapate.

Habari zilizolifikia gazeti hili zinadai kwamba baadhi ya wazazi wameshaliwa mapesa kibao baada ya kuingizwa mjini na matapeli hayo.

Kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, watu hao walikwenda shuleni kwao na wakaowaorodhesha majina ya wanafunzi kibao kwa ajili ya dili hilo .

Amesema licha ya wao kuwa na mashaka lakini walikuwa wakisisitizwa kuwa wameshirikishwa walimu wao na hivyo kuwataka wasiwe na wasiwasi na badala yake wakazungumze na wazazi wao ili waweze kuandaliwa kwenye kundi hilo.

``Walikuja shule vijana wawili wakidai kuwa wanaweza kututengenezea alama za kufaulu kwenye mitihani yetu , na kwamba wao wametumwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani na baadhi yetu wakajiandikisha,`` alisema mwanafunzi huyo.

``Mzee sisi tunafanya dili hizi kwa muda mrefu tukishirikiana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, lakini kwakuwa yeye ni mtu mkubwa, anatutumia sisi kuzungumza na walimu, wanafunzi pamoja na wazazi,`` alisema mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Yona wakati akiongea na Alasiri, akidhani ni mmmoja wa wateja wake.

Aidha Alasiri ilipozungumza na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Unity Commecial ya Jijini, Bw. Macksenzius Kihwili ambayo inatuhumiwa kushiriki dili hilo, alikanusha vikali.

Akizungumza na Alasiri ofisini kwake, Bw. Kihwili alisema ameshtushwa na taarifa hiyo na kusema kwamba shule yake haina uhusiano na matapeli hao.

``Mimi kwakweli sijui kama kuna watu wamekuja hapa shuleni kwa nia ya kufanya mchezo huo, ila kama upo, labda utakuwa unafanywa na walimu wa chini na nitafuatilia hili kwa umakini,`` alisema Bw. Kihwili.

  • SOURCE: Alasiri
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.