|
Kanisa lamwaga viti kibao kwa walemavu nchini
2008-02-26 15:43:40
Na Abdul Mitumba, Sinza
Uongozi wa Kanisa la Christian Mission Fellowship la Sinza Jijini limelazimika kuongeza misaada yake ya viti kwa walemavu wa maeneo mbalimbali nchini baada ya kubaini kuwa idadi ya walengwa ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa hapo awali.
Awali, kanisa hilo lilitenga viti vya magurudumu matatu zaidi ya 2000 ili kugawa kwa walemavu , lakini imelazimika kuagiza viti vingine maradufu kutoka China ili kuwafikia walemavu wengi zaidi.
Kiongozi wa kanisa hilo, Askofu Mgulla Kilimba, ameyasema hayo juzi katika hafla ya kukabidhi msaada wa viti 50 kwa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, Bw. Vita Kawawa.
Amesema kanisa limelazimika kutoa viti hivyo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 7.5 ili kusaidia jitihada za Serikali katika kuwasaidia walemavu.
``Lengo letu ni kuhakikisha kuwa walau katika kipindi cha miaka kumi ijayo, nchi yetu isiwe na mlemavu anayesota chini kwa kukosa nyenzo za kumsaidia kutembelea,`` amesema.
Akasema idadi ya viti vya walemavu vilivyotolewa kuanzia mwaka uliopita hadi sasa ni 1,100.
Viti hivyo vimeshambazwa katika majimbo tisa nchini na pia katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI.
Akizungumza baada ya kupokea viti hivyo, Mheshimiwa Kawawa alisema analishukuru kanisa hilo kwa kuwasaidia walemavu, hasa wa jimbo lake akisema kwake hiyo ni bahati ya kipekee.
``Nasema hii ni bahati ya kipekee kwa walemavu wangu wa Namtumbo kwa sababu Tanzania ina majimbo mengi na walemavu wengi, hivyo kitendo cha kanisa kulipa viti hivi jimbo hili ni kama bahati kubwa kwangu,`` amesema.
|