|
Waziri Mkullo awatoa presha waliokuwa wakurugenzi Wizara ya Mipango, Uchumi
2008-02-26 15:44:57
Na Anneth Kagenda, POSTA
Kufuatia kuvunjwa kwa iliyokuwa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji na kuwa wizara moja ya Fedha na Mambo ya Uchumi, Serikali imewatoa hofu wakurugenzi wa iliyokuwa wizara hiyo baada ya matumbo yao kuwaka moto wakihofia kupoteza vibarua vyao.
Wanene hao waliokuwa wakikuna vichwa usiku na mchana wakifikiria hatma ya vyeo vyao, wameelezwa kuwa wataendelea kufanya kazi kwa nyadhifa hizo hadi pale Rais Kikwete atakaposaini mfumo mpya wa uendeshaji wa wizara hiyo mpya ya fedha na Mambo ya Uchumi.
Hofu hiyo imetolewa jana na Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Bw, Mustafa Mkullo, wakati alipokuwa akizungumza na waajiriwa wa wizara hiyo nyeti.
Kabla ya kuwatoa hofu hiyo, Waziri huyo alitoa nafasi ya Wakurugenzi hao kujitambulisha na ndipo kila mmoja aliposimama na kujitambulisha kuwa mimi ni fulani bin fulani, niliyekuwa Mkurugenzi wa idara .
Kitendo hicho kilimfanya waziri na wageni waliokuwapo wakiwemo waandishi wa habari kuangua kicheko na baadaye waziri kulazimika kutoa ufafanuzi uliowaondoa hofu waliyokuwa nayo.
Akawaambia badala ya kujawa na hofu, wafanye kazi kwa kujituma zaidi, hasa ile ya kuandaa bajeti.
Akasema Bw. Mkullo kuwa wizara hiyo ina wasomi wengi kuliko iliyokuwa Wizara ya Fedha, hivyo si rahisi serikali ikawatosa.
``Hapa watu wana digrii zao mbilimbili... leo hii uwapunguze utawapeleka wapi? Na kwa nini ichukuliwe hatua hiyo? Kuanzia sasa, sitaki muwe na wasiwasi... msijiite aliyekuwa Mkurugenzi. Endeleeni kujiita vilevile, kama wewe ni Mkurugenzi, jiite hivyohivyo na wala si aliyekuwa ,`` akasema Bw. Mkullo.
``Si sahihi kuanza kufikiria kuwa hamna kazi, hatutegemei kati yenu wasomi nyie mkakosa kazi, huwezi kumtoa mtu mwenye digrii mbili ukamuweka mwingine,``
Akasema idara zilizopo na kazi zilizopo zitafanya kazi kama zilivyo na kwamba haamini kuwa miongoni mwao kuna ambaye ataondolewa kwenye nafasi yake.
``Tuko katika kuandaa bajeti mpya , tunahitaji mchango wenu mkubwa, nyie ni wasomi msikae mkawaza mnapunguzwa. Msikonde bure... ondoeni mawazo, chapeni kazi,`` akasisitiza Waziri Mkullo na kuwafanya vigogo hao wapate faraja.
Akiwa katika wizara ya fedha, aliwataka waajiriwa hao kushughulikia malalamiko ya pensheni kwa wakati muafaka.
Akasema akiwa wizarani hapo, ameshuhudia malalamiko mengi ambayo yametokana na ukosefu wa majibu mazuri kwa wastaafu hao.
|