26 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mwakyembe yu hatarini
 
2008-02-26 15:49:00
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Serikali imeombwa kumpatia ulinzi Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mchakato wa utoaji zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kampuni hewa ya Richmond, Dokta Harrison Mwakyembe na wajumbe wake ili wasifanyiziwe na watu walioguswa kwa njia moja ama nyingine na sakata hilo.

``Kama watu wamediriki kutoa kauli zinazodhihirisha wazi kuwa wana kinyongo na kamati ya Dk. Mwakyembe, basi wanayopanga kuyafanya kwa siri yanaweza kuwaweka wana kamati hao hatarini,`` mkazi mmoja wa Jijini ameliambia gazeti hili.

Mtu mwingine aliyeonyesha wasiwasi juu ya usalama wa Dk. Mwakyembe na timu yake ni Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party, TLP, Bw. Agostine Mrema.

Ameliambia gazeti hili leo asubuhi kuwa kitendo cha baadhi ya watu walioguswa na matokeo ya uchunguzi wa kamati hiyo, kutoa kauli zenye kinyongo na kumwaga shutuma waziwazi, sio dalili njema, kwa vile inaonyesha kuwa wana chuki zao binafsi.

``Mimi naamini kazi ya Dk. Mwakyembe na kamati yake ilikuwa safi, kwani kuandika ripoti kama ile ilihitajika ujasiri mkubwa sana, lakini hawa walioanza kuitupia lawama, inaonyesha dhahiri kuwa watuhumiwa wameumia na wana chuki binafsi dhidi ya kamati hiyo,`` akasema Bw. Mrema.

Bw. Mrema amesema kutokana na chuki hiyo, ni dhairi kuwa maisha ya Dk. Mwakyembe na wajumbe wa kamati yake yako hatarini, kwa kuwa watuhumiwa hao wanaweza kutumia fedha na raslimali zao kuwadhuru.

Aidha Bw. Mrema amesema ikiwa watuhumiwa hao wanaona kamati haikuwatendea haki, zipo taratibu za kwenda kulalamika Bungeni au kushtaki mahakamani na wala sio kwa waandishi wa habari au kwenye uchochoroni.

Akasema watuhumiwa waliotajwa na Kamati ya Richmond, ambao hivi sasa wanavitumia vyombo vya habari kuichafua kamati ya Dk. Mwakyembe, wanapaswa kukemewa kwa vile wanarudisha nyuma vita dhidi ya ufisadi.

Mkazi mwingine wa Jijini aliyejitambulisha kwa jina la Hana Emmanuel amesema kitendo cha watuhumiwa kutoa matamshi ya kudhalilisha hadharani kinaonyesha wanajiamini mno na hakuna anayejua jeuri hiyo wanaipata wapi.

``Mimi napinga matamshi yao yanayolenga kuidhalilisha Kamati ya Bunge, tukiacha hili liendelee, hata kamati nyingine zitaleta ripoti za kuwabeba watuhumiwa kwa kuchelea kudhalilishwa,`` akasema Bi. Hana.

Mkazi mwingine wa Jijini aliyejitambulisha kwa jina la Masoud Maulid, ameshauri Serikali iangalie namna ya kuwalinda mashujaa hao, kwa kuwapa walinzi.

``Si lazima wawe na mabodigadi wa kuonekana, inaweza kuangaliwa njia ya kuwawekea ulinzi wa siri,`` akashauri Bw. Masoud.

Akizungumzia vita dhidi ya ufisadi, Bw. Mrema amesema Rais Kikwete alianza vizuri vita hiyo lakini akamtaka kuongeza nguvu ili kuhakikisha mafisadi wanamalizwa nguvu moja kwa moja.

Kauli hiyo imekuja wakati ni leo tu, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji, TIC, Bw. Emmanuel Ole Naiko amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kamati hiyo imemhusisha na kashfa hiyo ya Richmondi, kwa kumuonea kwa vile yeye pia kama alivyo Bw. Lowassa ni mzaliwa wa wilayani Monduli.

Naye Bw. Bw. Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri Mkuu kutokana na kashfa hiyo, amesikika mara kadhaa akiilaumu kamati ya Dk. Mwakyembe kwa kushindwa kumpa nafasi ya kujitetea.

Bw. Lowassa aliporudi jimboni kwake aliandaliwa mapokezi makubwa na kutandikiwa zulia jekundu kama ishara ya ushujaa wake.

Akiwa jimboni kwake, Bw. Lowassa alifanya mkutano wa hadhara na kuwaambia wananchi kuwa yeye hahusiki na kashfa hiyo isipokuwa aliwajibika kutokana na makosa ya watu wengine.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.