17 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wanafunzi wa sekondari mbili Kigamboni wadundana
 
2008-03-17 19:01:38
Na Moshi Lusonzo, Jijini

Wanafunzi watano wanadaiwa kujeruhiwa na wengine watatu kudakwa na Polisi baada ya kuzuka mapigano katika shule zao za Kidete na Aboud Jumbe zilizopo Kigamboni, Kata ya Mjimwema.

Imeelezwa kuwa chanzo cha mapigano hayo ni kutambiana kwa uwezo wa kifedha baina ya wanafunzi wa shule hizo.

Akizungumza na Alasiri, Diwani wa Kata hiyo, Bi. Lilian Rweyemamu, amesema mapigano hayo yalianza taratibu na kudumu kwa kipindi cha wiki moja, lakini siku ya Jumatatu ndiyo iliyokuwa balaa kwani wanafunzi hao walipigana zaidi na kusababisha magari kushindwa kupita kutokana na madereva kuhofia mawe yaliyokuwa yakirushwa hovyo.

Diwani Lilian anasema kwa mujibu wa mashuhuda, wanafunzi hao walikuwa wakitumia zana mbalimbali zikiwemo za bisibisi, nyembe na visu, hivyo kuwafanya baadhi yao kujeruhiwa vibaya.

Hata hivyo, akasema kutokana na juhudi za Polisi, vurugu hizo zilitulizwa.

Akizungumzia hali ilivyokuwa, Diwani Lilian akasema chanzo cha ugomvi huo ni kitendo cha wanafunzi wa Kidete kuwaita wenzao wa Abdu Jumbe kuwa ni akina kayumba kutokana kuwa hawana gari la kuwapeleka na kuwarudisha shuleni kwao.

``Unajua Shule ya kidete wana mabasi ya kuwapeleka na kuwarudisha shuleni yanayogharimiwa na wazazi wao, tofauti na wanafunzi wa Aboud Jumbe ambao hawana... sasa kila wanapowaona wenzao wamesimama barabarani wakisubiri usafiri, wale wa Kidete wanawaita wenzao Kayumba na ndipo utani huo ukazaa mapigano,`` akasema diwani huyo.

Imeelezwa kuwa siku ya Alhamisi, baadhi ya wanafunzi wa shule hizo wakakutana ufukweni majira ya saa 8:30 alasiri na hapo ndipo ugomvi mkubwa ulipozuka kati ya wanafunzi hao na kuendelea hadi siku ya pili yake ambapo wanafunzi kadhaa walijeruhiwa kwa kuchomwa na bisibisi na kupigwa visu.

Inaelezwa kuwa kufuatia hali hiyo, polisi waliitwa tena na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi watatu wanaodaiwa kuwa vinara wa mapigano hayo.

Pamoja na hayo, katika kikao cha dharura kilichoitishwa mara baada ya kutokea mapigano hayo na kuwahusisha viongozi wa shule hizo mbili, polisi na diwani wa kata hiyo, yalitolewa maazimio ambayo yatafuatwa na wanafunzi hao wakati masuala mengine yakiendelea kufanyiwa kazi.

Aidha, akasema wanafunzi wa shule hizo wamepigwa marufuku kwenda ufukweni kupumzika kwa kuwa huko imebainika ndio chanzo cha mgogoro huo.

Hata hivyo, mwandishi hakuweza kupata taarifa ya polisi kuhusiana na tukio hilo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.