|
Polisi wa vituo vya Hananasif wachongewa kwa DC K`ndoni
2008-03-17 19:02:29
Na Abdul Mitumba, Hananasif
Askari Polisi katika mkoa maalum wa Kinondoni wameanzishiwa zengwe la aina yake na wananchi baada ya kudai kuwa baadhi ya askari wake wamegeuza vituo vyao vya kazi kama sehemu ya miradi ya kujipatia fedha kutoka kwa watuhumiwa.
Aidha, askari hao wamesema hatua hiyo ya baadhi ya askari polisi inasababisha vitendo vya uhalifu kuongezeka hasa katika maeneo ambayo idadi ya polisi katika vituo vilivyopo ni kidogo kulinganisha na ukubwa wa eneo na uhitaji wa huduma zao.
Madai hayo yametolewa na baadhi ya wananchi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Hananasif mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Fabian Massawe.
Mmoja wa wananchi hao, Bw. Stephen Gwaka, amemueleza DC Massawe mbele ya hadhara hiyo kuwa, licha ya kata yao ya Hananasif kuwa na vituo viwili vya polisi, bado inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa askari wa kutosha na mbaya zaidi, waliopo wamegeuza vituo vyao vya kazi kama miradi ya kujipatia fedha.
``Inashangaza kuona vitendo vya uhalifu ni vingi katika kata yetu na wahalifu wengi wanajulikana… kila kukicha wanakamatwa, lakini baada ya muda mfupi wanaonekana tena mitaani,`` amesema.
``Kwakweli inasikitisha… ukihoji kwa nini hali inakuwa hivi utasikia wakitamba kuwa mtu akiwa na pesa hawezi kufanywa lolote,`` akaongeza.
Aidha, Bw. Gwaka ambaye alikuwa akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo, ikiwa kama ishara ya kuunga mkono malalamiko hayo, akasema kauli hizo zinazidisha kiburi cha watuhumiwa wa uporaji dhidi ya raia wema na wakati mwingine, kutengeneza mazingira magumu raia kutoa taarifa za siri kwa polisi juu ya vitendo vya kihalifu.
Malalamiko ya mwananchi huyo na wengineo yalikuja baada ya diwani wa kata hiyo, Bw. Abbas Tarimba, kusoma taarifa nzuri juu ya mafanikio yaliyopatikana na kata katika suala la ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kukarabatiwa kwa vituo viwili vya polisi vya kata hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo, DC Massawe aliagiza wananchi kwa kushirikiana na ofisi ya Mtendaji Kata kuweka mitego ya rushwa ili kuwanasa polisi hao haraka iwezekanavyo.
Bw. Massawe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Kinondoni, amesema vitendo vya rushwa kamwe havikubaliki na akatoa namba yake ya simu ya mkononi ili atakayepata taarifa za kuwepo kwa vitendo hivyo amjulishe mara moja.
Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Bw. Massawe aliwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii huku wakizingatia sheria zilizopo ili kujiletea maendeleo yao wenyewe.
|