17 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Vijana 45 toka Bongo kuhamia Ruvu kulima mpunga
 
2008-03-17 19:03:18
Na Valery Kiyungu, Mabibo

Vijana wapatao 45, wakazi wa mtaa wa Jitegemee kata ya Mabibo Jijini Dar es Salaam, wanatarajia kuondoka kwenda Ruvu mkoani Pwani kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo cha zao la mpunga, baada ya kupatiwa mashamba katika eneo hilo la bonde la Ruvu.

Akizungumza na Alasiri ofisini kwake, mwenyekiti wa mtaa wa Jitegemee, Bw. Omary Chikoya amesema vijana hao wameangukiwa na ngekewa hiyo kufuatia maombi waliyotuma kwa wenyeji wa Ruvu wakitaka wapatiwe maeneo ya kulima mpunga.

Amesema kwa mujibu wa taarifa ya kukubaliwa kwa maombi hayo iliyofikishwa katika ofisi yake, vijana wake hao wamepatiwa pori kubwa la ekari 20, katika eneo moja lililoko kwenye bonde la mto Ruvu mkoani Pwani.

Hata hivyo amesema walionufaika wa mpango huo ni wale ambao wameanzisha vikundi maalum vya maendeleo kwenye mtaa huo wa Jitegemee, kwa ajili ya kujiajiri wenyewe kufuatia kukosekana kwa ajira.

Mwenyekiti huyo wa mtaa huo ulioko katika Manispaa ya Kinondoni amevitaja vikundi vya vijana hao kuwa ni Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Mabibo, TAMAVIMA, Yapoko na kikundi cha Amani, ambavyo vyote vina makazi yake hapo mtaa wa Jitegemee.

Amesema vijana hao hivi sasa wako katika pilika pilika ya kusaka wataalam wa kilimo ili kuweza kuwapa ushauri zaidi juu ya kilimo hicho cha zao la mpunga.

Amesema hii ni mara ya kwanza katika mtaa wake vijana kuamua kuhama Jijini kwenda kujishughulisha na kilimo.

Bw. Chikoya amewataka vijana wengine kujiunga na kujaribu kufanya shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato kwa njia halali badala ya kubweteka kutokana na kukosekana kwa ajira.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.