|
Manispaa Kinondoni yatoa Sh. Mil. 5 kusaidia yatima
2008-03-17 19:03:59
Na Abdul Mitumba, Mikocheni
Yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu 200 wa Kata za Mikocheni na Magomeni, Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar, wamenufaika na msaada wa vifaa vya shule vyenye thamani ya Sh. Milioni 5.
Kata hizo zimepokea vifaa hivyo kutoka Manispaa ya Kinondoni kupitia mpango wake wa kusaidia yatima katika kata zote 27 za Manispaa hiyo kupitia ofisi za madiwani na watendaji wa kata.
Ofisa mtendaji wa kata ya Mikocheni, Bi. Elizabeth Mbalali amesema jana kuwa kata yake imepata kiasi cha Sh. Milioni 2.5 ambazo zimetumika kununulia vifaa vya shule kwa watoto 100, ikiwa ni pamoja na mabegi, sare, na mikebe.
Akizungumza katia hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, diwani wa kata hiyo Bw. Harold Maruma, amesema fedha za kununulia vifaa hivyo zimetolewa na Manispaa ya Kinondoni kupitia kamati yake ya kudhibiti ukimwi.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Magomeni, Bi. Latifa Ramadhan, akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa yatima wa kata yake, amesema fedha zilizotumika kununulia vifaa hivyo ni matunda ya watu kulipa kodi mbalimbali.
Akizungumzia msaada huo, Diwani wa Kata hiyo, Bw. Julian Bujugo, amesema pamoja na Manispaa kutoa fedha za kununulia vifaa hivyo, lakini pia inatoa wito wa kuitaka jamii kushirikiana na Serikali katika kuwatunza yatima hao.
Amesema yatima hao 100 waliopata vifaa hivyo katika kata yake ni sehemu ya watoto 170 wanaotambuliwa na Serikali ambapo hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, idadi yao ilikuwa 120, lakini katika kipindi cha Januari na Februari mwaka huu wameongezeka na kufikia 170.
|