|
Risasi zatembea sheli, mmoja hoi
2008-03-17 19:04:54
Na Moshi Lusonzo, Jijini
Mfanyakazi mmoja wa kituo cha Mafuta cha Tanita kilichopo mjini Kibaha, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa hoi baada ya kupigwa risasi wakati majambazi walipovamia kituo chao hicho hivi karibuni.
Mfanyakazi huyo anayefahamika kwa jina la Ali Sufiani, 35, mkazi wa Tabata Jijini, sasa amelazwa katika wodi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili, MOI, baada ya risasi hizo kumvunja mguu.
Akizungumza huku akiwa hoi wodini, Bw. Sufiani ambaye ni dereva wa lori la kubebea mafuta, akasema tukio hilo limemtokea majira ya saa 2:00 usiku, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akasema katika tukio hilo, majambazi hayo yalikuwa yakitumia bunduki ya kivita, ambapo mara tu yalipovamia, yalianza kuungurumisha risasi kila mahali ili kuwaogopesha wananchi wasiende kutoa msaada.
Aidha, akasema majambazi hao waliwalazimisha kuonyesha sehemu iliyohifadhiwa pesa.
Akasema walipokataa, ndipo walipoanza kumwaga risasi na kumvunja mguu wake wa kulia kwa risasi mbili.
Baada ya hapo, akasema majambazi hayo yakafanikiwa kuingia katika chumba cha kuhifadhia fedha na kuchukua mauzo yote ya siku hiyo kabla ya kuingia mitini.
Kwa mujibu wa Afisa uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa, mtu huyo alifikishwa hospitalini kwao majira ya usiku, akitokea Kibaha ambapo juhudi za kumpatia matibabu zinaendelea.
Hata hivyo, akasema hadi sasa, tayari wameshamfanyia upasuaji na kuunga mfupa wake uliovunjika.
|