|
Waganga wa Jadi wataka Sheria ya Uchawi iwekwe wazi kuzuia mauaji
2008-05-05 18:23:06
Na Abdul Mitumba, Jijini
Serikali imeombwa kuweka wazi jinsi sheria ya uchawi inavyofanya kazi ili kuwaondolea wananachi wake utata wa namna ya kushughulikia masuala hayo yanayotokana na imani za kishirikina.
Hivi sasa, Serikali bado inatambua kuwepo kwa sheria ya Uchawi ya mwaka 1926, `Witchcraft Ordinance Act`, ambayo ni namba 18, kifungu cha pili.
Sheria hiyo inafafanulia, kuaminisha na kujumuisha ulozi, kuganga na kugangwa, matumizi ya vifaa vya kichawi, kumiliki na kutumia na njia za kutenda maajabu na miujiza.
Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na Chama cha Waganga wa Tiba Asilia Tanzania, CHAWATIATA Jijini Dar, Serikali inapaswa kulifanyia kazi suala hilo mapema ili kuondokana na matendo kama yaliyojiri sasa Dar na pia namna ya kuyakabili kisheria.
Mwenyekiti wa CHAWATIATA Jijini, Dk. Maneno Tamba, amesema kuwa matukio ya hivi karibuni Jijini yameonyesha umuhimu wa kutekelezwa kwa wazo hilo.
``Lengo langu siyo kuzungumzia kuwepo kwa matukio hayo, lakini nataka kujaribu kueleza juu ya kukupa sheria hii ambayo serikali inaitambua hiyo inavyopaswa kuiboresha ili iendane na wakati uliopo,`` amesema.
Dk.Tamba pia amesema vitendo vya kuuawa kwa albino, ni aina nyingine ya imani hatari ambazo zinapaswa kukomeshwa na ndio maanchama chake kinaamini kuwa sasa, Serikali inapaswa kufanya jambo fulani, likiwemo hilo la kuuelimisha umma kuhusu sheria husika.
Hivi sasa, tukio la mtoto Ramadhan Mussa, 12 kudaiwa kukutwa akikifyonza damu kichwa cha mtoto mwingine aitwaye Salome Yohana, 3, limekuwa gumzo Jijini na polisi wamesmhikilia mtuhumiwa huku uchunguzi mkali ukiendelea.
|