|
Yamewakuta!
2008-05-05 18:32:53
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Upepo mbaya unazidi kuwafunika baadhi ya vigogo wa CCM waliohusishwa na tuhuma mbalimbali. Licha ya kuvua nafasi walizokuwa nazo za uwaziri, bado wametakiwa kubwaga manyanga na kuachia nafasi zote za uongozi walizo nazo ndani ya chama.
Wakizungumza na Alasiri, baadhi ya wakazi wa Jijini wamesema kama maazimio hayo ya vijana wa CCM mkoani Tanga yatatekelezwa kivitendo, ni wazi kwamba mawaziri hao waliojiuzulu watakuwa na wakati mgumu kisiasa, kwani inaweza kuchukua muda mrefu kabla jamii kuanza kuwaamini tena.
``Kweli viongozi hawa waliojiuzulu sasa yamewakuta... endapo tamko la vijana hao wa Tanga litapata sapoti ya wana CCM wengine, ni wazi kwamba watapata kazi kubwa ya kukubalika upya mbele ya wananchi,`` akasema Bw. Henry Raphael mkazi wa Sinza.
Naye Bw. Hassan Jamal wa Kijitonyama amesema ameshangazwa na ujasiri wa vijana hao wa CCM mkoani Tanga, ambao wamenukuliwa leo na vyombo mbalimbali vya habari wakiwataka viongozi waliojiuzulu wabwage pia nafasi wanazoshikilia ndani ya chama na pia zile za ubunge.
``Inashangaza. Sikuwahi kusikia maoni ya namna hii hapo kabla. Lakini, naamini hii ndio faida ya demokrasia ndani ya CCM... na kama wazo lao litatekelezwa, wahusika watakuwa wameathirika mno kisiasa,`` akasema.
Leo, Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), mkoa wa Tanga, wamekaririwa wakitoa tamko la kutaka viongozi wa Serikali waliojiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali waachie ngazi kwenye nafasi za uongozi ndani ya chama ili kukinusuru chama na chuki zitokanazo na tuhuma zinazowakabili.
Tamko la umoja huo lililosomwa kwa waandishi na Mwenyekiti wa UVCCM ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Uenezi na Siasa mkoani humo, Bw. Emmanuel Kiondo.
Vijana hao wakabainisha kuwa walioachia nafasi zao serikalini bado wamebaki wakipeta na madaraka makubwa ndani ya chama hicho, jambo wanalodai kuwa ni hatari katika kujenga imani kwa umma.
Wakasema viongozi hao hawana budi kutafakari upya na kupima kama bado wanaheshima ya kusiamama mbele ya jamii na kisha kunadi sera bora na Ilani ya CCM.
Akasema wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, wabunge hata Kamati za Maadili .
Viongozi waliojiuzulu nafasi zao hivi karibuni kutokana na kuhusishwa na tuhuma mbalimbali ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Monduli Bw. Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki Dk. Ibrahim Msabaha, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bw. Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge.
|