|
Diwani Kurasini adai manispaa Temeke imepoteza mamilioni
2008-05-07 19:41:06
Na Moshi Lusonzo, Jijini
Manispaa ya Temeke Jijini imekosa zaidi ya Shilingi Milioni 74 kufuatia nyumba zake nane na kiwanja kuuzwa kinyemela.
Akiongea na waandishi wa habari jana, Diwani wa Kata ya Kurasini ambapo nyumba na kiwanja hicho kipo, Bw. Wilfred Kimatti amesema pesa hizo zingepatikana kutokana na fidia kama Manispaa hiyo ingehusika kuuza kiwanja hicho.
Akasema kutokana na sakata hilo, kuna kundi la watu limeanza kuibuka na kuanza kuwachafua wenzao na kuacha ukweli wa nani aliyehusika kwa uuzwaji wa kiwanja hicho kilichopo katika `ploti` namba 366, ndani ya kata hiyo.
Bw. Kimatti akaeleza kuwa ofisi yake haijahusika na uuzwaji wa eneo hilo kwa kuwa haingwezekana kuhusika kuuza kiwanja chenye pesa za namna hiyo, tena kilicho chini ya WIzara ya Ardhi.
``Katika tathmini ya awali, ilibainika kuwa eneo hilo lilikuwa na thamani zaidi ya shilingi milioni sabini... hili ni jambo kubwa na kama kuna watu wanaanza kuchafuana kwa kumtafuta mchawi, watakosea hasa ikiwa mchawi mwenyewe anafahamika,`` akasema.
Akasema kuna watu kutoka Wizara ya Ardhi ndio walioipa kampuni moja ya mafuta hati ya kumiliki eneo hilo.
Diwani Kimatti akasema katika hatua zote zilizofanyika katika uuzwaji wa kiwanja hicho kwa kampuni hiyo ya mafuta, ofisi yake pamoja na ofisi ya Serikali za Mitaa haikuhusika kwa namna yoyote ile.
Kufuatia kuibuka kwa sakata hilo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Luteni Abdallah Kihato, amewapa siku 21 Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Stephen Kongwa na Meya Bw. Jerome Bwanausi kuwasaka watu wote waliohusika na uuzwaji wa kiwanja hicho na kuwachukulia hatua kali.
|